Wednesday, November 13, 2013

  Kwanza kabisa kila mtanzania kwa sasa anajua na kulisikia sana neno hili la "Big Results Now" Matokeo makubwa sasa. Mfumo huu serikali imeamua kuuchukua kutoka nchi ya Malaysia ambako ilionekana kuwanufaisha na kukuza uchumi wao kwa haraka. Hebu tuziangalie hizi nchi mbili sasa.

Wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961, nchi ya Malaya ilikuwa tayari ina uhuru mwaka 1957. Malaya ilijiunga na Singapore, Sabah na Sarawak mwaka 1963 na kuunda Malaysia. Tanganyika yenyewe ilijiunga Zanzibar 1964 kuunda Tanzania. Hata hivyo Singapore ilifukuzwa katika muungano huo mwaka 1965. Nchi zote hizi mbili zilitawaliwa na Mwingereza.

  Wakati Tanzania inaundwa mwaka 1964, pato la wastani la mtu mmoja lilikuwa ni USdolar 63, wakati Malaysia ilikuwa USdolar 113. Kimsingi nchi hizi zilikuwa sawa kimaendeleo ingawa Tanzania ni kubwa mara tatu ya Malaysia.

  Hivi sasa Malaysia kipato cha wastani cha mwananchi ni USdolar10,000 na Tanzania ni USdolar 600. Kwa Tanzania pato limeongezeka mara kumi na Malaysia limeongezeka mara elfu moja.
Nini tofauti ya mikakati ya nchi hizi mbili?

  Leo hebu tuangalie eneo moja tu la Kilimo, na namna Kilimo kilivyoweza kuivusha nchi ya Malaysia na Kilimo hicho hicho bado hakijaweza kuivusha Tanzania.
Malaysia iliunda Shirika la Umma, Federal Land Development Authority, (FELDA) likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wananchi masikini wanapata ardhi, wanlima kisasa na kuongeza uzalishaji, kisha kufuta umasikini.

  Kila mwananchi masikini aligawiwa hekta 4.1, ardhi ikasafishwa na kuwekewa miundombinu ya muhimu, ikapandwa michikichi na mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi hiyo. Shughuli zote hizi zilifanywa kwa gharama za Serikali na wananchi wote waliowezeshwa wakapewa kama mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza Mawese kwa Shirika hili la Serikali. Hivi sasa Shirika hili ni kubwa sana, lina thamani USdolar bilioni 3.5 na kupitia ushirika wao wananchi hawa waliopewa ardhi ya kulima michikichi sasa wanamiliki 20% ya Shirika hili.
Malaysia iliweza kuondoa umasikini kutoka 57% ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1965 mpaka chini ya 3% mwaka 2012.

  FELDA sasa ni Shirika la Kimataifa maana linaanza kuwekeza duniani kote. FELDA ilipouza hisa zake kwenye masoko ya mitaji, IPO yake ilikuwa ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Facebook na Japanese Airlines. Shirika la Umma linalomilikiwa na Serikali, Wakulima na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (EPF) na linaloendeshwa kwa misingkini ya utawala wa Makampuni limeweza kufuta umasikini kwa zao moja tu la Michikichi. Malaysia leo inaongoza kwa kuuza Mawese duniani. Michikichi hiyo ilitoka Tanzania na kupelekwa  Malaya na waingereza miaka ya hamsini.

  Tanzania nasi tulikuwa na Shirika la Umma kwa ajili ya Kilimo. Tuchukulie Shirika la NARCO kama FELDA, NARCO walichukua ardhi kubwa maeneo kadhaa nchini. Tofauti na FELDA wao walilima wenyewe mashamba haya na kuweka miundombinu ya Kilimo.
Tuchukulie mfano wa mashamba ya mpunga kule Kapunga, wilaya ya Mbalali Mkoa wa Mbeya. Mwaka 1985 NARCO walikwenda kijijini Kapunga kuwaomba wananchi wawape ardhi ya kulima mpunga. Wananchi wakawapa hekta 3000 hivi. NARCO wakapata msaada kutoka katika Serikali ya Japani na uwekezaji mkubwa ukafanyika ikiwemo kuweka kinu cha kukoboa mpunga cha kisasa kabisa.

  Hata hivyo NARCO ilijiendesha kwa hasara na ilipofika katikati ya miaka ya 90 ikaamriwa kubinafsishwa. NARCO ikauza mashamba yale kwa mpango wa ubinafsishwaji kwa Makampuni binafsi. Katika uuzaji huo NARCO waliuza hekta 3500 badala ya 3000 walizopewa na wananchi, kwa maana hiyo kijiji cha Kapunga nacho kiliuzwa.

  Mifano hii miwili inaonyesha tofuti kubwa za kifikra kimaendeleo kati ya nchi zetu hizi mbili. Moja iliwezesha wananchi kumiliki ardhi na imefanikiwa. Na nyingine iliamua kufanya kupitia Shirika la Umma na baada ya kushindwa, badala ya kurejesha ardhi kwa wananchi na kuwawezesha kulima, ardhi ile ikauzwa kwa kampuni ya mtu mmoja. Mfano wa Kapunga uko pia huko wilayani Hanang kwenye mashamba ya Ngano ya Basotu n.k.

  Hata kwenye mpango wa SACGOTT bado fikra ni za wakulima wakubwa wenye mashamba makubwa badala ya kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi na kulima kwa mfumo ambao huduma zitatolewa kwa pamoja. Ujamaa wa Malaysia ulikuwa ni wa kumilikisha wananchi wao ardhi na kuwawezesha kuzalisha.
UJamaa wetu ulikuwa ni wa kumiliki kwa pamoja na hivyo kukosa uwajibikaji. Badala ya kuboresha na kuwawezesha wakulima wadogo wadogo, wakubwa wanaona ni bora kwwenda kwa wakulima wakubwa na kugawa ardhi hovyo bila mpango.

  Kwa mantiki hiyo kweli "Big Results Now" itafanikiwa? Kosa ninaloliona mimi hapa, Serikali imechukua mfumo huu kutoka Malaysia ambao wao wliweka mpango dhabiti na kuuandikikia kitabu wakikiita  "Big Fast Results" huku wakiweka miundombinu ya kutosha kuuwezesha mpango kutimia. Wakati sisi tunaoiga mfumo huu tunataka" matokeo makubwa sasa" lakini hatuna mipango ya kupata hayo matokeo sasa.

Je, hatuwezi kujifunza kwa wenzetu kweli?  Lini tutaacha Umazwazwa?

  
 

1 comments:

  1. CONTACT: onlineghosthacker247 @gmail. com
    -Find Out If Your Husband/Wife or Boyfriend/Girlfriend Is Cheating On You
    -Let them Help You Hack Any Website Or Database
    -Hack Into Any University Portal; To Change Your Grades Or Upgrade Any Personal Information/Examination Questions
    -Hack Email; Mobile Phones; Whatsapp; Text Messages; Call Logs; Facebook And Other Social Media Accounts
    -And All Related Services
    - let them help you in recovery any lost fund scam from you
    onlineghosthacker Will Get The Job Done For You
    onlineghosthacker247 @gmail. com
    TESTED AND TRUSTED!

    ReplyDelete