Friday, April 18, 2014

Ndugu zangu wakulima, wadau wote wa kilimo na wasomaji wa mtandao huu. Tunaelekea kwenye mavuno sasa ambapo sehemu mbalimbali ama wameanza au wako kwenye mavuno.
Katika mchakato wa uvunaji, ni kipindi cha kuwa makini sana maana unaweza ukazalisha vizuri lakini ukaja kupoteza kiasi kikubwa wakati wa mavuno.

Katika kuhakikisha kwamba mazao yanakuwa katika ubora na hali nzuri kwa mlaji (consumer), wadau katika mchakato huu lazima waunganishe nguvu za pamoja. Hebu tuwatambue wadau hawa na wajibu na majukumu yao katika mchakato huu.

(i) Mkulima
(ii) Serikali
(iii) Maafisa Ugani
(iv) Wauza Pembejeo (Stockissts)

Wajibu wa Mkulima

- Kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo.
- Kuvuna na kuandaa mazao
- Kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu.
- Kuwasilisha matatizo yao kwa wagani ili waweze kujadiliana jinsi ya kuyatatua.
- Kutumia mbinu za kienyeji zenye kuleta mafanikio.
Wajibu wa Serikali

- Kutunga na kusimamia sheria na sera (mfano sheria ya Dumuzi)
- Kuwawezesha wagani kuwasaidia wakulima (mafunzo)
- Kufanya utafiti
- Kutoa ruzuku au mikopo midogo midogo kwa ajili ya kuendeleza hifadhi ya mazao.
- Kutunga na kusimamia Sera ya Masoko.

Wajibu wa Wagani

- Kuwatembelea Wakulima na kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali na jinsi ya kuzitatua.
- Kuwaunganisha wakulima na watoa huduma mbalimbali.
- Kuunganisha wakulima na watafiti.

Wajibu wa wauza Pembejeo

- Kuwauzia wakulima Pembejeo bora ikiwa ni pamoja na viuatilifu vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaostahili
- Kutoa elimu kwa wakulima.

MAANA HALISI YA UHIFADHI NA UPOTEVU WA MAZAO.

* Uhifadhi ni kitendo cha kuweka mazao yako sehemu maalum kwa muda maalumu kabla ya kuuzwa au kutumika.

* Upotevu wa mazao ni hali ya kupungua thamani kwa mazao kutokana na sababu mbalimbali kama vile kusinyaa, kunyauka, kuliwa na wadudu, kuibiwa au kupotea.

Madhumuni ya kuhifadhi

. Kwa ajili ya chakula
. Kwa ajili ya biashara
. Kwa ajili ya biashara
. Kwa ajili ya mbegu

AINA YA UPOTEVU WA MAZAO.

Upotevu wa mazao unaweza kutokea kwa namna mbalimbali kama:

1. KUPUNGUA UZITO

Kuna aina nyingi za visababishi na vingi ni vile vinavyokula mazao hasa wadudu na wanyama kama Panya. Aidha uvunaji usio na umakini huacha mazao mengi shambani na hivyo uhifadhi kuanza na kiasi pungufu kuliko ilivyokusudiwa.

2. KUPUNGUA KWA UBORA

Visababishi vikuu ni wadudu wanaokula, wanaochafua, au shughuli inayovunja au kuharibu punje, kuchafua mazao kwa aina yoyote au kuoza, kusinyaa, kutoa harufu n.k

3. UPOTEVU WA VIINI LISHE

Visababishi vikuu ni vile vinavyokula viini vya punje ambavyo ndivyo vyenye virutubisho na vitamini. Kadhalika hifadhi duni.

4. UPOTEVU WA MAPATO

Hutokana na yote yaliyotajwa hapo juu ambapo matokeo yake ni zao kupata ndogo kwenye soko na hivyo uchumi wa mkulima kuwa duni.

5. UPOTEVU WA NGUVU YA UOTO KWENYE MBEGU.

Visababishi ni hifadhi duni na vyote vilivyotajwa hapo juu.

Katika mzunguko mzima wa uvunaji, kuna ngazi mbalimbali za upotevu ambazo ni;

- Kuvuna
- Kusafirisha
- Kukausha
- Kupukuchua/kupura
- Kupepeta/kuchambua
- Kupanga madaraja
- Kuweka dawa ya kuua wadudu
- Kuhifadhi kwenye vifaa au maghala
- Kutumia kwa chakula au kuuza
- Kusinsika.

Hebu basi tujadili sasa njia za kuweza kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvuna.

DHANA SHIRIKISHI YA UDHIBITI WA VISUMBUFU.

Aina za wadudu waharibifu:

i. Dumuzi
ii. Fukusi wa mahindi
iii. Mende mwekundu wa unga
iv. Wadudu jamii ya nondo/vipepeo
v. Visumbufu wengine ni wanyama waharibifu wakiwemo Panya.

UDHIBITI WA VISUMBUFU AINA YA WADUDU.

. Udhibiti kwa njia ya asili (Cultural control)
. Udhibiti kwa kutumia viuatilifu (Chemical control)
. Udhibiti kwa kutumia nguvu ya binadamu (Physical control)
. Udhibiti husishi (Intergrated Storage Management)

Katika udhibiti kwa njia ya viuatilifu, inatakiwa mkulima awe mwangalifu kuangalia viuatilifu sahihi na viwango vya kutumia. Kadhalika matumizi salama ya viuatilifu na tahadhari yatasisitishwa.

Mambo mengine muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika matumizi ya viuatilifu ni pamoja na;

. Kukauka kwa nafaka
. Usafi wa nafaka
. Kuchambua nafaka
. Kugawa zao
. Viwango sahihi
. Kutumia viuatilifu ambavyo havijakwisha muda wake
. Usafi na hali ya ghala au vyombo vya kuhifadhia
. Ukaguzi wa mara mara wa nafaka na ghala.

Sasa tuangalie jinsi ya ktumia viuatilifu aina ya vumbivumbi. Kabla ya kuanza shughuri nzima ya kutumia kiuatilifu (dawa), mambo muhimu ya kuzingatia ni;

(i) Kuhakikisha ni kiuatilifu kilichopendekezwa na wataalamu

(ii) Kusoma lebo na kufuata maelekezo kwa usahihi

(iii) Jinsi ya kupima na kujua kiwabgo kilachoshauriwa

(iv) Jinsi ya kuhakikisha kwamba nafaka imekauka kwa kiwango kinachostahili

(v) Kuzingatia mwelekeo wa upepo wakati wa kutumia

(vi) Jinsi ya kusafisha magunia au vyombo vingine kabla ya kuvijaza nafaka

(vii) Mambo ya kuzingatia katika kuondokana na vifungashio vilivyokwisha kiuatilifu pamoja na viuatilifu vinavyobaki.

(viii) Tahadhari za kiafya wakati wa kutumia viuatilifu.

Jinsi ya kutumia viuatilifu aina ya majimaji kutayarisha ghala.

Zoezi hili litazingatia mambo yafuatayo ;

(i) Tofautisha matumizi ya viuatilifu vya majimaji na vile vya vumbivumbi katika hifadhi.

(ii) Jinsi ya kuchanganya kiuatilifu cha majimaji kupata kiwango kinachostahili.

(iii) Matumizi sahihi ya mabomba ya kunyunyizia viuatilifu.

Njia mbadala kwa madawa ni kutumia vifaa visivyoingiza hewa kama vile mapipa.

Udhibiti wa Panya

Panya ni visumbufu katika kundi la wanyama, hushambulia zaidi mazao ya nafaka kuanzia shambani hadi ghalani na hupunguza kipato cha mkulima kwa kiwango kikubwa asipo dhibitiwa. Ili kuweza kumdhibiti Panya ni lazima;
- Ujue tabia za Panya

- Ujue jinsi ya kutambua maeneo wanakopita.

- Ujue sumu za Panya (sumu za kizazi cha kwanza na za kizazi cha pili).

Ujue namna sahihi ya utegaji wa Panya.

Note: aina hizo za dawa yaani kizazi cha kwanza na kizazi cha pili, kizazi cha kwanza ni dawa ambayo inaua Panya peke yake na kizazi cha pili ni ile dawa ambayo inaua mtambuka pale ambapo kuku akimdonoa Panya aliye kufa, na huyo Kuku atakufa kutokana na hiyo dawa. Zipo hadi kizazi cha tatu ingawa ni mara chache ambapo binadamu au mbwa akimula huyo Kuku, atakufa.

Kwa hiyo ndugu zangu wakulima na wote mnaotembelea kwenye blog hii, tujitahidi kadri tuwezavyo kukabiliana n upotevu huu.

2 comments: