Tuesday, May 13, 2014

Habari za siku mbili tatu ndugu zangu wakulima na wadau wote wa kilimo. Poleni na shughuri za kilimo hasa uvunaji maana sasa ni kipindi cha mavuno.

Katika mchakato wa kilimo kuna wadau wengi wanaohusika katika kuhakikisha kwamba mkulima ananufaika na kilimo kwa kuongeza tija kwenye uzalishaji na katika kuongeza kipato chake na kupanua pato la taifa kwa ujumla.

Mojawapo ya wadau wanaofanya kazi moja kwa moja na kwa ukaribu na mkulima ni Watafiti, ambao kazi yao kubwa ni kutafiti uwezekano wa kuongeza kipato katika uzalishaji kwa kutumia njia mbali mbali ambazo zitaleta tija mashambani.

Kuna vituo vingi vya utafiti hapa nchini ambapo walau kila kanda ina kituo cha utafiti. Ili mkulima aweze kuzalisha mazao ya kutosha, hana budi kushirikiana kwa karibu na watafiti ili kuweza kuendana na chochote kinachotolewa na watafiti katika kuendeleza kilimo chake.

Kituo cha utafiti uyole ni jituo kinachohudumia nyanda za juu kusini, katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa. Katika Mradi wa AGRA, kitengo cha Afya ya Udongo ( Soil Health Project) kinachosimamiwa na Kituo cha Utafiti Uyole chini ya Mtafiti William Mmari na timu yake, wameweza kufanya kazi moja kwa moja na wakulima kwa kuwashirikisha Wagani na Wakulima wenyewe kwa pamoja.

Katika Mradi huu mbinu mbali mbali za uzalishaji zinatumika na wakulima wenyewe ndio wanaohusika na kushiriki moja kwa moja shambani.

Katika kubadilishana uzoefu kwenye maeneo yanayosimamiwa na mradi, watafiti wamefanya ziara kubwa ya kutembeleana ambapo lengo kuu ni kujaribu kuonyesha uhalisia wa matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao.

Mbolea ya Minjingu Mazao imekuwa na changamoto nyingi sana tangu kuingia kwake sokoni. Imeweza kutekwa na wanasiasa na kuiondolea uhalisia wake. Mbolea hii haikufanya vizuri ilipoingia sokoni, na yawezekana kwa sababu ya elimu duni waliyokuwa nayo wakulima katika matumizi ya Mbolea hiyo. Baada ya kuonekana hivyo watengenezaji wa Mbolea hiyo waliamua kuiongezea virutubusho zaidi na kuibadilisha jina na sasa inaitwa Minjingu Mazao.

Serikali imeamua kuwatumia Watafiti na Wagani kwa kutumia mashamba darasa. Katika mashamba darasa ya Mradi kwa kweli yamefanya vizuri kwa kutumia Minjingu Mazao kama yanavyoonekana kwenye picha hapo juu. Wakulima waliohudhuria walishuhudia na kuamini.

Mbolea hii si mbaya kama inavyochukuliwa na baadhi ya wanasiasa na wakulima. Lakini kitaalamu ni Mbolea nzuri na ina faida za ziada kwenye udongo. Inaweza kuonekana haina ubora endapo mkulima hatafuata kiwango halisi cha uwekaji kwenye shamba.

Matumizi ya mbolea yoyote yanasimama kwenye kiwango cha kutumia shambani. Minjingu inatakiwa 120kg kwa ekari moja au kwa hesabu ya rahisi kwa mkulima ni mifuko 2 kwa ekari. Kosa lililofanyika mwanzo mwanzo ni uelewa wa wakulima wa jinsi ya kutumia Mbolea hii. Walikuwa wakitumia kwa mazoea ya DAP ambayo hutumika 50kg ama mfuko mmoja kwa ekari na matokeo ni kushindwa kukidhi hitaji kwa mmea.

Pia katika kutembeleana kwenye ziara hii ambapo nami nilikuwa mmoja wapo, tulitembelea katika mashamba ya vijiji viwili katika kata ya Isansa wilaya ya Mbozi ambavyo ni Isansa na Mpito. Na katika kijiji cha Mpito tuliweza kutembelea shamba la Mkulima mmoja ambaye alihudhuria kama shuhuda wa Minjingu Mazao ambapo amelima shamba lake la takribani eka 2 na robo tatu hivi kwa kutumia mbolea ya Minjingu Mazao na akakuzia mkuzio wa kwanza kwa kutumia Minjingu mazao hiyo hiyo na mkuzio wa pili akatupia kidogo UREA mifuko 2 tu. Matokeo katika shamba hili ni mazuri na yanaridhisha sana.

Wito wangu kwa wakulima ni kwamba mnashauriwa kufuata ushauri wa wataalam katika kutumia Pembejeo.

Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Afisa Kilimo na Mifugo.

1 comments:

  1. CONTACT: onlineghosthacker247 @gmail. com
    -Find Out If Your Husband/Wife or Boyfriend/Girlfriend Is Cheating On You
    -Let them Help You Hack Any Website Or Database
    -Hack Into Any University Portal; To Change Your Grades Or Upgrade Any Personal Information/Examination Questions
    -Hack Email; Mobile Phones; Whatsapp; Text Messages; Call Logs; Facebook And Other Social Media Accounts
    -And All Related Services
    - let them help you in recovery any lost fund scam from you
    onlineghosthacker Will Get The Job Done For You
    onlineghosthacker247 @gmail. com
    TESTED AND TRUSTED!

    ReplyDelete