Saturday, May 24, 2014

KAHAWA BORA

Ubora wa kahawa ndio uti wa mgongo kwa upatikanaji wa bei nzuri. Ili mkulima apate bei nzuri, ni muhimu azingatie kanuni zote kilimo bora cha kahawa. Kwa kufanya hivyo, atakuwa amejijengea mazingira imara ya kuzalisha kahawa ya madaraja ya juu itakayompatia bei nzuri.

Mambo ambayo mkulima anatakiwa kufanya ili apate kahawa bora ni;

1. Kuheshimu na kutekeleza kanuni zote za kilimo bora cha kahawa, bila kuruka mojawapo.

2. Vivyo hivyo, ni budi kuzingatia kanuni zote za utayarishaji wa kahawa, kuanzia hatua ya kuvuna shambani, hadi inapopelekwa kwenye kituo cha mauzi.

Leo katika Makala hii nitajielekeza zaidi kueleza na kufundisha kanuni za utayarishaji bora wa kahawa kuanzia hatua ya uvunaji. Mkulima hana budi kuelewa kwamba atakuwa amejenga na kuimarisha msingi mzuri kwa ubora wa kahawa yake iwapo atakuwa makini katika kutekeleza kanuni zote za kilimo bora cha kahawa. Hali kadhalika kwa kuwa mwangalifu katika kutayarisha kahawa kabla haijauzwa, mkulima atakuwa analinda na kuhifadhi ubora ambao umeshajengeka. Kufanya vinginevyo atakuwa anavuruga mafanikio ya kazi nzuri ya awali.

Sifa nzuri ya kahawa inatambulika kirahisi kwa sura, umbo, uzito wa punje, na kadhalika kwa uonjo/ladha yake. Sifa hizi zinajengeka au kuharibika kutokana na uimara au udhaifu wa matunzo shambani. Kahawa hupangwa katika madaraja mbalimbali kulingana na vigezo hivyo vya ladha, sura, umbo na uzito wa punje.

(i) Madaraja ya kahawa ni; kutoka juu kwenda chini ( kunakoambatana na kupungua kwa thamani) AA, A, PB na C kulingana na kiwango cha sifa zilizotajwa hapo awali.

(ii) Kahawa ya madaraja ya chini AF, TT, T na F ni nyepesi licha ya kupungukiwa na sifa nyinginezo za kahawa bora katika madaraja ya juu.

Ni dhahiri kwamba, kahawa ya mkuluma aliyezingatia kanuni zote za kilimo bora, itakuwa katika madaraja ya juu na atapendelea kutunza na kuhifadhi ubora huo ili apate bei nzuri zaidi.

Lengo la kuhifadhi ubora wa kahawa litafikiwa kwa kutekeleza kwa uangalifu kanuni zote bora za utayarishaji wa kahawa.

KANUNI ZA UTAYARISHAJI BORA WA KAHAWA NGAZI YA MKULIMA.

KUCHUMA; Hakikisha unachuma matunda yaliyoiva ambayo ni mekundu sawasawa.
Usichume zile zenye rangi nusu-nyekundu nusu-njano au ya mchanganyiko wa kijani kibichi. Ikiwa hizo zimechumwa kwa bahati mbaya, zitengwe kabla ya kuanza zoezi la kumenya, la sivyo zitaharibu ladha na sura ya kahawa baadaye.

KUMENYA; Kahawa imenywe siku ile ile inapochumwa, kuhakikisha kuwa ile sukari iliyo kwenye ganda la nje haipenyezi ndani hadi kwenye punje, kwa kuwa itaharibu uonjo. Mashine ya kumenyea iwe safi na irekebishwe vizuri ili isije ikaminya punje. Tumia maji mengi na safi wakati wa kumenya. Ni vyema buni zimwagwe kwenye maji na kukorogwa ili zile nyepesi na zilizo haribika zielee. Hizo ziondolewe ziwekwe kando ili zimenywe peke yake. Maelea yote yaondolewe na kushughulikiwa peke yake. Baada ya kumenywa kahawa isafishwe kiasi na maelea yote yaondolewe.

KUVUNDIKA; Hatua hii ni ya kuondoka ute (mscilage) unaozunguka kila kila punje. Baada ya kusafisha kahawa iliyomenywa, ni muhimu ivundikwe katika matangi masafi yaliyo yaliyotengenezwa kwa saruji. Vifaa vya Aluminium/ chuma kama vile masufuria, pia vinafaa. Kamwe usitumie vifaa vya mbao. Kahawa ilundikwe pamoja na kusonganishwa na siyo kutandazwa. Kahawa hiyo ifunikwe kwa gunia safi ili isifikiwe na mwanga wa jua au mvua. Kahawa ivurugwe mara kwa mara ili yote iweze kuvunda kwa pamoja. Yafaa kufanya hivyo walau mara mbili kwa siku.

Baada ya masaa 24, kahawa hiyo ioshwe kwa maji kwa maji yanayotiririka na ifunikwe tena. Hakuna muda wa kanuni wa kuivundika kahawa. Tofauti za hali ya hewa katika maeneo tofauti huharakisha au kuchelewesha kahawa kuvunda. Uvundikaji wa kahawa huwa umekamilika pale punje ikibonyezwa kwa vidole hukwaruza, na ule ute unaonatanata unakuwa umetoweka. Vinginevyo kutokamilika kwa uvundikaji au kuvunda nusunusu kutaifanya kahawa yako kuwa na ladha/uonjo, harufu na sura ngeni ambayo vinachangia sana katika kupungua kwa ubora wa kahawa.

KUSAFISHA; Safisha kahawa kwa kutumia maji safi na panga katika madaraja. Ondoa punje nyepesi na masalia yote ya maganda. Hakikisha unasafisha kahawa yako vizuri hadi ute wote unaonatanata umeisha kwenye punje. Kahawa yako sasa iko tayari kuanikwa.

KUANIKA NA KUPANGA KATIKA MADARAJA.

(a) Kuanika

Baada ya kusafishwa, kahawa ianikwe kwenye chekecheke zilizoinuliwa kiasi cha meta moja kutoka usawa wa ardhi. Ardhi chini ya chekecheke iwekwe katika mazingira safi. Kamwe nyasi zisiachwe kuota kukaribia chekecheke.

Sambaza kahawa kwenye chekecheke katika kina cha inchi moja. Hakikisha unyevu unanyauka na kuisha kwenye ngozi ya punje (skin drying). Siku ya kwanza kuanika endelea kuvurugavuruga kwenye chekecheke na kuifunika kahawa vipindi vya jua kali sana ili isikauke kupita kiasi na pia kuizuia kupata vumbi. Ikiwezekana, baada ya ngozi ya juu kukauka, hamishia kahawa kwenye jafafa (kitambaa cha gunia- hessian cloth). Utagundua kuwa kahawa yako imekauka vizuri utakapobonyeza punje kwa vidole isibonyee, na rangi ya punje kubadilika na kuwa nusu kijani na nusu kijivu. Ukitumia chombo cha kupimia unyevu kitaonyesha unyevu usiozidi 13% kwenye punje.

(b) Kupanga katika madaraja.

Katika ngazi hii, hatua hii ni ya awali tu. Wakati kahawa ikiendelea kukauka, ondoa buni, punje zilizo na mabaki ya maganda na zilizobadilika rangi. Pia ondoa zilizo nyepesi na zile zilizo babuka zitunzwe na hatimaye kuuzwa pekee.

KUHIFADHI GHALANI

Kahawa sasa iwekwe kwenye magunia safi na kuhifadhiwa katika ghala safi na lenye nafasi ya kutosha kuruhusu mwanga na mzunguko wa hewa.

Kwenye ghala, magunia ya kahawa yapangwe juu ya mbao zilizoinuliwa ili yasigusane na ardhi. Hakikisha ghala halivuji maji na wala halina hali ya unyevu. Kamwe ghala lisiwe na bidhaa nyingine zozote kama vyakula, viungo vya chakula, madawa ya mimea au ya mifugo.

Kahawa ipelekwe kwenye kituo cha mauzo katika mazingira hayo hayo ya usafi.

MWISHO

Mkulima atakayezingatia kanuni kwa makini atakuwa amezalisha kahawa bora na kuitunza vizuri hivyo kujihakikishia bei nzuri.

Kwa kuwa uzalishaji wa kahawa duniani unaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, njia pekee ya kuboresha mapato yetu ni kuongeza uzalishaji na kuendelea na jitihada za kuimarisha na kulinda ubora wa kahawa yetu.

Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi kwa ushirikiano na Tanzania Coffee Board, TCB.

1 comments:

  1. CONTACT: onlineghosthacker247 @gmail. com
    -Find Out If Your Husband/Wife or Boyfriend/Girlfriend Is Cheating On You
    -Let them Help You Hack Any Website Or Database
    -Hack Into Any University Portal; To Change Your Grades Or Upgrade Any Personal Information/Examination Questions
    -Hack Email; Mobile Phones; Whatsapp; Text Messages; Call Logs; Facebook And Other Social Media Accounts
    -And All Related Services
    - let them help you in recovery any lost fund scam from you
    onlineghosthacker Will Get The Job Done For You
    onlineghosthacker247 @gmail. com
    TESTED AND TRUSTED!

    ReplyDelete