Wednesday, September 28, 2016

KILIMO BORA CHA UFUTA

UTANGULIZI

Ufuta (simsim/sesame) ni zao la kibiashara ambalo mbegu zake zina kiasi kikubwa cha mafuta kiasi cha asilimia 45 hadi 55.Na zao hili linaweza kulimwa maeneo mengi ya Afrika mashariki na Tanzania.Ni zao ambalo linatowa mafuta yenye thamani kubwa na hivyo kulifanya zao bora la biashara.

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA

Zao hili linawezwa kulimwa katika maeneo yanayopata mvua kidogo.Maeneo ya ukanda wa chini kutoka usawa wa bahari hufaa zaidi kwa kilimo cha ufuta.Pia nyanda za juu ambazo ni chini ya mita 1500 hufaa kwa kilimo cha ufuta.Mfano kwa Tanzania unaweza Ukalima ufuta katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Manyara, Dodoma, Iringa na mkoa mpya wa Songwe katika maeneo ya bonde la Songwe wilaya mpya ya Songwe.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA.

Ufuta ustawi vizuri katika maeneo yenye udongo mwepesi mweusi na usiotuamisha maji,udongo tifutifu ni mzuri kwa kilimo cha ufuta,Pia ufuta unawezwa kulimwa katika udongo wowote lakini usiotuamisha maji.Ufuta hufa haraka kama maji yatatuama kwa muda mrefu shambani.

AINA ZA UFUTA

Kuna aina kuu mbili za mbegu za ufuta:

1) MBEGU ZA ASILI

Wakulima wengi hupanda mbegu za asili, mbegu ambazo zilianza kulimwa miaka mingi iliyopita.Mbegu hizi nyingi zina mavuno kidogo, kati ya 300kg-500kg kwa ekari na huchukua muda mrefu kukomaa Huchukua siku 140 hadi 180.

2) MBEGU ZA KISASA

Mbegu hizi zinakomaa kwa muda mfupi na hutowa mavuno mengi, wastani wa 500kg hadi 800kg kwa ekari kama shamba litaandaliwa, litapandwa na litatunzwa vizuri. Mbegu hizi huchukua siku 105 hadi 140 kukomaa.Mfano wa mbegu hizi ni Naliendele 92,Lindi 202,Ziada 94 na Mtwara 2009.

UPANDAJI WA UFUTA

Shamba la ufuta ni budi likatuliwe na kulimwa vizuri kabla ya kupanda,hata hivyo pia unaweza kupanda bila kukatua lakini mavuno yatapungua kidogo. Inashauriwa kupanda ufuta kwa mistari kwa vipimo vifuatavyo. Sentimeta 50 kwa 10 au 50 kwa 20 kama utapanda kwa kutumia mistari ya kuchimba vijifereji vidogo katika mstari na kudondosha mbegu hizo katika vifereji hivyo (Drilling method) na kwa kuacha mche mmoja mmoja kwa kila shina.
Pia sentimeta 50 kwa 30 au 60 kwa 30 kwa kuacha miwili kwa kila shina. Kwa Mbegu ya Asili Unaweza Kupanda kwa sentimeta 70 kwa 30 kwa Kuacha Miwili kwa Kila shimo.Fukia mbegu kwa sentimenta 2.5 hadi 5.

MUDA WA KUPANDA

Muda mzuri wa kupanda ufuta ni mwanzoni mwa msimu wa kilimo yaani Mwishoni mwa mwezi November hadi katikati kwa mwezi Januari.

MATUMIZI YA MBOLEA

Ufuta ni zao ambalo halihitaji matumizi makubwa ya Mbolea.Japokuwa hustawi zaidi katika udongo wenye rutuba ya kutosha.Kama utapanda katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha basi unaweza kutumia mbolea kiasi kidogo Mbolea kama vile UREA na BOOSTER.

MATUNZO NA PALIZI

Miche ya ufuta ni midogo na laini sana hivyo inahitaji palizi mapema hasa katika kipindi cha majuma manne ya kwanza. Pia katika kipindi hiki unatakiwa kupunguza miche iliyosongamana. Kadri utavyochelewesha palizi na kupunguzia mimea mapema ndivyo unavyoifanya mimea isikuwe vizuri na kujipunguzia kipato chako.

MAGONJWA YA UFUTA

Magonjwa makuu ya ufuta ni madoa ya majani na kuoza matawi na shina. Zuia magonjwa haya kwa Kupanda mbegu bora na kwa kutokupanda ufuta katika ardhi inayotuamisha maji, pia itawezekana kubadilisha shamba usilime ufuta katika shamba lililolimwa msimu uliopita.

WADUDU WANAOSHAMBULIA UFUTA

Kuna wadudu wengi wanaoshambulia ufuta kama vile vibaruti (Ambao hushambulia hatua ya mwanzo kabisa ya miche iliyoota ya ufuta ambapo vibaruti hula majani ya mwanzo ya mmea mara tu yanapojitokeza). Pia Aphids hushambulia ufuta kwa kufyonza maji katika majani ya mimea hivyo kupelekea kukauka kwa majani ya mmea.
Pia wapo funza wa majani ambao hula majani ya mimea na pia hufunga majani ya ncha ya mimea na kuzuia ukuaji wa matawi wa mimea,wadudu hawa ni hatari zaidi kwani wanazuia kutengenezwa kwa vitumba vya ufuta.

Kuzuia vibaruti:

Kabla hujapanda mbegu yako changanya na dawa ya tunza au gaucho. Pia panda mbegu bora na fanya mzunguko mazao shambani. Wadudu wengine wakijitokeza tumia dawa kama karate, dimethoate, Twigathoate, duduall, duduba na dawa nyingine za wadudu kabla wadudu hawajasababisha madhara makubwa shambani.

UVUNAJI

Ufuta uliokomaa tayari kwa kuvunwa utaonesha mabadiliko ya majani yake na shina na matawi yatabadilika rangi yake na kuwa njano au kahawia au yataanza kukauka,pia vitumba vya mwanzo vitaanza kubadilika rangi yake na kuanza kukauka hivyo utatakiwa ukate ufuta mapema kabla vitumba havijakauka na kupasuka.Vuna ufuta wako kwa kukata matawi ya ufuta na kuyafunga katika matita ya saizi inayokufaa ila yasiwe matita makubwa sana ambayo hayatakauka katikati kwa urahisi yasimamishe matita yako kuelekeza juu kisha acha yakauke kwa wiki mbili hadi nne kutegemea na ukali wa jua.vitumba vikisha kauka na kupasuka tandika mkeka au turubai na yageuze matita yako katika mkeka na turubai hapo ufuta utamwagikia katika mkeka au turubai lako,kuupata ufuta unaokwama katika matita piga piga kidogo tita unapoligeuza. Kisha Peta ufuta wako na kuuweka katika Vyombo safi vya kuhifadhia.

SOKO

Soko la ufuta kwa kiwango kikubwa kinauzwa nje ya nchi, matumizi ya ndani ni machache sana. Na hasa wanunuzi wakubwa ni India na wauzaji wakubwa kwa ukanda wetu huu ni wakenya, ndo ma exporter wakubwa ingawa inawezekana hata hawazalishi kiwango kikubwa cha ufuta kutuzidi. Kipindi cha mavuno bei ya ufuta hufikia hadi 1800/= kwa kilo na ukiadimika hufikia hadi 2200/= kwa kilo na dumu la lita 20 hufikia hadi kilo 18.

Prepared by

Marcodenis E. Misungwi

Agriculture Extensionist.

Tuesday, September 27, 2016

KILIMO BORA CHA MCHICHA

Mchicha ni mboga za majani na maua yake hutumika katika kutengeneza mchuzi rojorojo. Mbegu za mchicha ni chakula safi kwa watoto wachanga. Mbegu husagwa na kutengenezwa uji na zaidi ya hayo pia mchicha huweza kumwongezea mkulima kipato.

MAHITAJI YA HALI YA HEWA KWAAJILI YA KULIMA MCHICHA.
Mchicha unahitaji maji ya kutosha katika kipindi chake chote cha ukuaji hadi kuvuna. Vilevile mchicha huhitaji udongo wenye rutuba ya kutosha na wenye kuhifadhi maji.

UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Tengeneza shamba la mchicha kwa kutifua ardhi na kulainisha udongo wenye kina cha sentimeta thelathini. Weka mbolea ya samadi debe moja katika kila mita moja ya mraba. Panda mchicha katika matuta yenye upana wa 90cm-100cm.

AINA ZA MBEGU

· Amaranthus hybridus huu ni mchicha wenye majani mekundu na mbegu zake ni nyeusi.

· Amarantus africana ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni ni nyeusi.
· Amaranthus hypochondriacus ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni njano hasa mbegu zake hutumika kutengeneza uji wa watoto wachanga.

· Amaranthus dubius ni mchicha wa kienyeji na Aspinosus ni mchicha wenye miba mingi.

UPANDAJI
· Changanya mbegu za mchicha na mchanga kwa uwiano wa 1:3, 1:4, 1:5 au 1:6 ili kurahisisha upandaji.
· Mchicha upandwe katika tuta kwa mistari yenye nafasi ya sentimita thelathini.

· Funika mbegu kwa kutumia udongo uliolaini na tandaza nyasi kavu baada ya kupanda ili kutunza unyevunyevu na toa matandazo baada ya siku tatu hadi tano tangu siku ya kupanda.

· Pandikiza mchicha kwa nafasi ya sentimeta kumi na tano kwa ishirini.
· Mwagilia maji ya kutosha.

KUKUZIA
Tumia mbolea ya samadi iliyolowekwa kwenye maji kwa muda wa masaa ishirini na nne kumwagilia mchicha wako ili kupata mavuno mengi zaidi. Tumia kiasi cha debe moja kwa kila mita moja ya mraba.

NAMNA YA KUDHITI WADUDU WAHARIBIFU

Adui mkubwa wa mchicha ni wadudu aina ya mafuta au kitaalamu zaidi huitwa spinach aphids ambao hufyonza utomvu wa mchicha na kusababisha majani kujikunja , mchicha kusinyaa na kunyauka. Kudhibiti wadudu hawa mwagilia mchicha wako kutumia chombo kinachotoa maji mithili ya mvua kitaalamu kinaitwa "watering can" ili kuwadondosha wadudu hao.

Wadudu wengine ni kitambazi ambacho hula majani ndani kwa ndani hivyo tumia mwarobani kunyunyuzia majani ili kuwaua wadudu hao waharibifu.

MAVUNO

Mchicha huwa tayari kuvunwa baada ya majuma 3 hadi 6 tangu kupandwa au kupandikizwa. Uvunaji huweza kuendelea kwa muda wa miezi 2 hadi 3 kutegemeana na namna utakavyoamua kuuvuna mchicha wako.

KIASI CHA MAVUNO

Kila mita moja ya mraba huzalisha kiasi cha 4kg hadi 5kg za mchicha. Hii inamaanisha kuwa utapata kiasi cha tani 20 hadi 40 kwa hekta moja ya mchicha.

NAMNA YA KUHIFADHI MCHICHA KWA SIKU NYINGI ZAIDI

· Baada ya kuvuna funga mashina ya mchicha na weka katika chombo chenye maji kwa kufanya hivyo unaweza kuhifadhi mchicha kwa muda wa masaa 24 yaani siku moja.

Ili kuhifadhi mchicha kwa zaidi ya miezi 4 fanya kama ifuatavyo:-

· Vuna mchicha wako kisha usafishe vizuri
· Funga katika mafungu.
· Chemsha maji mpaka yachemke.
· Tumbukiza mafungu ya mchicha katika maji yanayochemka kwa muda wa dakika 1 hadi 2.

· Kausha vizuri chini ya kivuli na utunze mchicha wako katika sehemu isiyo na unyevunyevu.

Hapo utakuwa na uhakika wa kuuza mchicha wako supermarket na kuusafirisha hata nje ya nchi.

Prepared by:

Marcodenis E. Misungwi

Agriculture Extensionist.

Monday, September 26, 2016

JINSI YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA VIFARANGA WADOGO

Leo nataka nikuonyeshe jinsi ya kutengeneza chakula cha vifaranga wadogo yaani wa wiki 1 hadi wiki 4.

Mahitaji muhimu katika utengenezaji wa chakula cha vifaranga kilo 100.

Pumba ya mahindi 40kg,

Mahindi ya kuparaza 10kg,

Mashudu ya alizeti 20kg,

Dagaa 24kg,

Unga wa mifupa 5 kg,

Chokaa 1/4kg,

Chumvi iliyo sagwa 1/2kg

Chikpremix 1/4kg.

Hayo ndio mahitaji muhimu katika uandaaji wa chakula cha vifaranga kilo 100.
Ndugu kumbuka kuwa unaweza kutengeneza chakula hicho kwa ajili ya vifaranga wako na pia unaweza pia ukafanya biashara ya kuuza chakula cha kuku kwa kuanza na hicho cha vifaranga wadogo, jua kuwa katika jamii sio kila mfugaji anaweza kutengeneza chakula cha kuku kuna wengine wanaweza lakini hawana mda wakutengeneza na pia kuna wengine hawajui kabisa jinsi ya kutengeneza, Ndugu msomaji wa mtandao huu ningependa utajirike na ufugaji kwa kuanzia na biashara ya uuzaji wa vyakula vya kuku. Leo anza kutengeneza hicho kwa kilo 100 unaweza kutengeneza ata kg 200kg, 300kg, 500kg ata 1000kg cha kufanya wewe ndiye unapaswa kuongeza mahitaji kwa kadri uwezavyo .

Prepared by:

Marcodenis E. Misungwi

Agriculture Extensionist.