Mtandao huu ni kwa ajili ya kuelimishana juu ya Kilimo na Mifugo na changamoto zake. Karibu tujifunze wote.
Thursday, May 29, 2014
SHAMBANI SOLUTIONS: WHY AGRICULTURE NEEDS YOUNG PEOPLE
Saturday, May 24, 2014
UANDAAJI WA KAHAWA BORA.
Ubora wa kahawa ndio uti wa mgongo kwa upatikanaji wa bei nzuri. Ili mkulima apate bei nzuri, ni muhimu azingatie kanuni zote kilimo bora cha kahawa. Kwa kufanya hivyo, atakuwa amejijengea mazingira imara ya kuzalisha kahawa ya madaraja ya juu itakayompatia bei nzuri.
Mambo ambayo mkulima anatakiwa kufanya ili apate kahawa bora ni;
1. Kuheshimu na kutekeleza kanuni zote za kilimo bora cha kahawa, bila kuruka mojawapo.
2. Vivyo hivyo, ni budi kuzingatia kanuni zote za utayarishaji wa kahawa, kuanzia hatua ya kuvuna shambani, hadi inapopelekwa kwenye kituo cha mauzi.
Leo katika Makala hii nitajielekeza zaidi kueleza na kufundisha kanuni za utayarishaji bora wa kahawa kuanzia hatua ya uvunaji. Mkulima hana budi kuelewa kwamba atakuwa amejenga na kuimarisha msingi mzuri kwa ubora wa kahawa yake iwapo atakuwa makini katika kutekeleza kanuni zote za kilimo bora cha kahawa. Hali kadhalika kwa kuwa mwangalifu katika kutayarisha kahawa kabla haijauzwa, mkulima atakuwa analinda na kuhifadhi ubora ambao umeshajengeka. Kufanya vinginevyo atakuwa anavuruga mafanikio ya kazi nzuri ya awali.
Sifa nzuri ya kahawa inatambulika kirahisi kwa sura, umbo, uzito wa punje, na kadhalika kwa uonjo/ladha yake. Sifa hizi zinajengeka au kuharibika kutokana na uimara au udhaifu wa matunzo shambani. Kahawa hupangwa katika madaraja mbalimbali kulingana na vigezo hivyo vya ladha, sura, umbo na uzito wa punje.
(i) Madaraja ya kahawa ni; kutoka juu kwenda chini ( kunakoambatana na kupungua kwa thamani) AA, A, PB na C kulingana na kiwango cha sifa zilizotajwa hapo awali.
(ii) Kahawa ya madaraja ya chini AF, TT, T na F ni nyepesi licha ya kupungukiwa na sifa nyinginezo za kahawa bora katika madaraja ya juu.
Ni dhahiri kwamba, kahawa ya mkuluma aliyezingatia kanuni zote za kilimo bora, itakuwa katika madaraja ya juu na atapendelea kutunza na kuhifadhi ubora huo ili apate bei nzuri zaidi.
Lengo la kuhifadhi ubora wa kahawa litafikiwa kwa kutekeleza kwa uangalifu kanuni zote bora za utayarishaji wa kahawa.
KANUNI ZA UTAYARISHAJI BORA WA KAHAWA NGAZI YA MKULIMA.
KUCHUMA; Hakikisha unachuma matunda yaliyoiva ambayo ni mekundu sawasawa.
Usichume zile zenye rangi nusu-nyekundu nusu-njano au ya mchanganyiko wa kijani kibichi. Ikiwa hizo zimechumwa kwa bahati mbaya, zitengwe kabla ya kuanza zoezi la kumenya, la sivyo zitaharibu ladha na sura ya kahawa baadaye.
KUMENYA; Kahawa imenywe siku ile ile inapochumwa, kuhakikisha kuwa ile sukari iliyo kwenye ganda la nje haipenyezi ndani hadi kwenye punje, kwa kuwa itaharibu uonjo. Mashine ya kumenyea iwe safi na irekebishwe vizuri ili isije ikaminya punje. Tumia maji mengi na safi wakati wa kumenya. Ni vyema buni zimwagwe kwenye maji na kukorogwa ili zile nyepesi na zilizo haribika zielee. Hizo ziondolewe ziwekwe kando ili zimenywe peke yake. Maelea yote yaondolewe na kushughulikiwa peke yake. Baada ya kumenywa kahawa isafishwe kiasi na maelea yote yaondolewe.
KUVUNDIKA; Hatua hii ni ya kuondoka ute (mscilage) unaozunguka kila kila punje. Baada ya kusafisha kahawa iliyomenywa, ni muhimu ivundikwe katika matangi masafi yaliyo yaliyotengenezwa kwa saruji. Vifaa vya Aluminium/ chuma kama vile masufuria, pia vinafaa. Kamwe usitumie vifaa vya mbao. Kahawa ilundikwe pamoja na kusonganishwa na siyo kutandazwa. Kahawa hiyo ifunikwe kwa gunia safi ili isifikiwe na mwanga wa jua au mvua. Kahawa ivurugwe mara kwa mara ili yote iweze kuvunda kwa pamoja. Yafaa kufanya hivyo walau mara mbili kwa siku.
Baada ya masaa 24, kahawa hiyo ioshwe kwa maji kwa maji yanayotiririka na ifunikwe tena. Hakuna muda wa kanuni wa kuivundika kahawa. Tofauti za hali ya hewa katika maeneo tofauti huharakisha au kuchelewesha kahawa kuvunda. Uvundikaji wa kahawa huwa umekamilika pale punje ikibonyezwa kwa vidole hukwaruza, na ule ute unaonatanata unakuwa umetoweka. Vinginevyo kutokamilika kwa uvundikaji au kuvunda nusunusu kutaifanya kahawa yako kuwa na ladha/uonjo, harufu na sura ngeni ambayo vinachangia sana katika kupungua kwa ubora wa kahawa.
KUSAFISHA; Safisha kahawa kwa kutumia maji safi na panga katika madaraja. Ondoa punje nyepesi na masalia yote ya maganda. Hakikisha unasafisha kahawa yako vizuri hadi ute wote unaonatanata umeisha kwenye punje. Kahawa yako sasa iko tayari kuanikwa.
KUANIKA NA KUPANGA KATIKA MADARAJA.
(a) Kuanika
Baada ya kusafishwa, kahawa ianikwe kwenye chekecheke zilizoinuliwa kiasi cha meta moja kutoka usawa wa ardhi. Ardhi chini ya chekecheke iwekwe katika mazingira safi. Kamwe nyasi zisiachwe kuota kukaribia chekecheke.
Sambaza kahawa kwenye chekecheke katika kina cha inchi moja. Hakikisha unyevu unanyauka na kuisha kwenye ngozi ya punje (skin drying). Siku ya kwanza kuanika endelea kuvurugavuruga kwenye chekecheke na kuifunika kahawa vipindi vya jua kali sana ili isikauke kupita kiasi na pia kuizuia kupata vumbi. Ikiwezekana, baada ya ngozi ya juu kukauka, hamishia kahawa kwenye jafafa (kitambaa cha gunia- hessian cloth). Utagundua kuwa kahawa yako imekauka vizuri utakapobonyeza punje kwa vidole isibonyee, na rangi ya punje kubadilika na kuwa nusu kijani na nusu kijivu. Ukitumia chombo cha kupimia unyevu kitaonyesha unyevu usiozidi 13% kwenye punje.
(b) Kupanga katika madaraja.
Katika ngazi hii, hatua hii ni ya awali tu. Wakati kahawa ikiendelea kukauka, ondoa buni, punje zilizo na mabaki ya maganda na zilizobadilika rangi. Pia ondoa zilizo nyepesi na zile zilizo babuka zitunzwe na hatimaye kuuzwa pekee.
KUHIFADHI GHALANI
Kahawa sasa iwekwe kwenye magunia safi na kuhifadhiwa katika ghala safi na lenye nafasi ya kutosha kuruhusu mwanga na mzunguko wa hewa.
Kwenye ghala, magunia ya kahawa yapangwe juu ya mbao zilizoinuliwa ili yasigusane na ardhi. Hakikisha ghala halivuji maji na wala halina hali ya unyevu. Kamwe ghala lisiwe na bidhaa nyingine zozote kama vyakula, viungo vya chakula, madawa ya mimea au ya mifugo.
Kahawa ipelekwe kwenye kituo cha mauzo katika mazingira hayo hayo ya usafi.
MWISHO
Mkulima atakayezingatia kanuni kwa makini atakuwa amezalisha kahawa bora na kuitunza vizuri hivyo kujihakikishia bei nzuri.
Kwa kuwa uzalishaji wa kahawa duniani unaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, njia pekee ya kuboresha mapato yetu ni kuongeza uzalishaji na kuendelea na jitihada za kuimarisha na kulinda ubora wa kahawa yetu.
Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi kwa ushirikiano na Tanzania Coffee Board, TCB.
Friday, May 23, 2014
KILIMO RAHISI CHA UYOGA KWA WAKULIMA WADOGO WADOGO.
Namna ya kuotesha Uyoga.
Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa Uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.
Hatua muhimu katika kuotesha Uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
. Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, Pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua n.k
Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea Uyoga.
. Mabua, Majani ya Mpunga au Migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sentimeta 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
. Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima ( saa 24).
. Kisha yachemshwe kwa muda wa saa 2 ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
. Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
. Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.
Namna ya kupanda.
Kuna aina mbili za upandaji;
AINA YA KWANZA
Chukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake.
Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.
Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa robo tatu ya mfuko.
NB: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.
AINA YA PILI
Changanya mali ghafi ya kuoteshea ( baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1:25 ( mbegu : mali ghafi ya kuoteshea).
Kwa uyoga aina ya Mamama ( Pleurotus spp), kisha mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni. Mifuko hii iwe ya ukubwa wa sm 20 kwa sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1-1.5 ya mali ghafi ya kutosha.
Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.
Zingatia:
(i) Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.
Uyoga ni Kiumbe hai, hivyo unahitaji kupumua.
(ii) Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hifadhi kwenye jokofu. Kama huna jokofu, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Mbegu za uyoga zinaweza kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
(iii) Waweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300 kwenye kilo 15 za mali ghafi ya kupteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
(iv) Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea. Vingine na hivyo haifai kupandwa.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Agriculture Extension Officer at Mbozi District Council.
MATUNZO YA ZAO LA UYOGA.
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza.
Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14-21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.
Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba cha mwanga na hewa ya kutosha kisichopigwa jua.
Katika chumba chenye mwanga. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye meza, chanja ya waya au miti. Mifuko pia inaweza kuning'inizwa kwenye kamba.
NB: Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko yaliyochemshwa na kupoa, mara tatu au zaidi kwa siku.
Tahadhari:
Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga.
Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa siku 2-3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.
UVUNAJI WA UYOGA.
Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa kuonekana.
Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung'oke.
Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwa kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.
Tuesday, May 13, 2014
ZIARA YA KUBADILISHANA UZOEFU KWA WAKULIMA KATIKA MRADI WA AGRA - AFYA YA UDONGO.
Katika mchakato wa kilimo kuna wadau wengi wanaohusika katika kuhakikisha kwamba mkulima ananufaika na kilimo kwa kuongeza tija kwenye uzalishaji na katika kuongeza kipato chake na kupanua pato la taifa kwa ujumla.
Mojawapo ya wadau wanaofanya kazi moja kwa moja na kwa ukaribu na mkulima ni Watafiti, ambao kazi yao kubwa ni kutafiti uwezekano wa kuongeza kipato katika uzalishaji kwa kutumia njia mbali mbali ambazo zitaleta tija mashambani.
Kuna vituo vingi vya utafiti hapa nchini ambapo walau kila kanda ina kituo cha utafiti. Ili mkulima aweze kuzalisha mazao ya kutosha, hana budi kushirikiana kwa karibu na watafiti ili kuweza kuendana na chochote kinachotolewa na watafiti katika kuendeleza kilimo chake.
Kituo cha utafiti uyole ni jituo kinachohudumia nyanda za juu kusini, katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa. Katika Mradi wa AGRA, kitengo cha Afya ya Udongo ( Soil Health Project) kinachosimamiwa na Kituo cha Utafiti Uyole chini ya Mtafiti William Mmari na timu yake, wameweza kufanya kazi moja kwa moja na wakulima kwa kuwashirikisha Wagani na Wakulima wenyewe kwa pamoja.
Katika Mradi huu mbinu mbali mbali za uzalishaji zinatumika na wakulima wenyewe ndio wanaohusika na kushiriki moja kwa moja shambani.
Katika kubadilishana uzoefu kwenye maeneo yanayosimamiwa na mradi, watafiti wamefanya ziara kubwa ya kutembeleana ambapo lengo kuu ni kujaribu kuonyesha uhalisia wa matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao.
Mbolea ya Minjingu Mazao imekuwa na changamoto nyingi sana tangu kuingia kwake sokoni. Imeweza kutekwa na wanasiasa na kuiondolea uhalisia wake. Mbolea hii haikufanya vizuri ilipoingia sokoni, na yawezekana kwa sababu ya elimu duni waliyokuwa nayo wakulima katika matumizi ya Mbolea hiyo. Baada ya kuonekana hivyo watengenezaji wa Mbolea hiyo waliamua kuiongezea virutubusho zaidi na kuibadilisha jina na sasa inaitwa Minjingu Mazao.
Serikali imeamua kuwatumia Watafiti na Wagani kwa kutumia mashamba darasa. Katika mashamba darasa ya Mradi kwa kweli yamefanya vizuri kwa kutumia Minjingu Mazao kama yanavyoonekana kwenye picha hapo juu. Wakulima waliohudhuria walishuhudia na kuamini.
Mbolea hii si mbaya kama inavyochukuliwa na baadhi ya wanasiasa na wakulima. Lakini kitaalamu ni Mbolea nzuri na ina faida za ziada kwenye udongo. Inaweza kuonekana haina ubora endapo mkulima hatafuata kiwango halisi cha uwekaji kwenye shamba.
Matumizi ya mbolea yoyote yanasimama kwenye kiwango cha kutumia shambani. Minjingu inatakiwa 120kg kwa ekari moja au kwa hesabu ya rahisi kwa mkulima ni mifuko 2 kwa ekari. Kosa lililofanyika mwanzo mwanzo ni uelewa wa wakulima wa jinsi ya kutumia Mbolea hii. Walikuwa wakitumia kwa mazoea ya DAP ambayo hutumika 50kg ama mfuko mmoja kwa ekari na matokeo ni kushindwa kukidhi hitaji kwa mmea.
Pia katika kutembeleana kwenye ziara hii ambapo nami nilikuwa mmoja wapo, tulitembelea katika mashamba ya vijiji viwili katika kata ya Isansa wilaya ya Mbozi ambavyo ni Isansa na Mpito. Na katika kijiji cha Mpito tuliweza kutembelea shamba la Mkulima mmoja ambaye alihudhuria kama shuhuda wa Minjingu Mazao ambapo amelima shamba lake la takribani eka 2 na robo tatu hivi kwa kutumia mbolea ya Minjingu Mazao na akakuzia mkuzio wa kwanza kwa kutumia Minjingu mazao hiyo hiyo na mkuzio wa pili akatupia kidogo UREA mifuko 2 tu. Matokeo katika shamba hili ni mazuri na yanaridhisha sana.
Wito wangu kwa wakulima ni kwamba mnashauriwa kufuata ushauri wa wataalam katika kutumia Pembejeo.
Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Afisa Kilimo na Mifugo.
Friday, May 2, 2014
KILIMO HIFADHI CHA MATANDAZO NA KUPANDA BILA KULIMA.
Uchumi wa soko huria umesababisha ongezeko kubwa la gharama za mbolea za viwandani, zana, madawa ya kuulia wadudu pamoja mbegu bora. Katika hali hii ni wazi wakulima ( hasa wadogo wadogo ) hawataweza kumudu ushindani iwapo wataendelea kutumia pembejeo za viwandani.
Uharibifu wa mazingira ( mmomonyoko wa ardhi, mgandamano wa udongo au udomgongo mfu ) unachangiwa na ongezeko la watu pamoja na gharama kubwa ya zana na pembejeo. Tunalazimika kubadilisha mtazamo wetu juu ya mazingira na mfumo sahihi/endelevu wa Kilimo. Zipo njia za asili za kurutubisha udongo na vilevile Kilimo cha jadi cha kutunza mazingira.
Wakulima wanashauriwa kupunguza utegemezi wa mbolea za viwandani kwa kujitengenezea mbolea yao wenyewe mashambani kwa kupanda na kufunika ardhi kwa mimea ya mikunde.
MATANDAZO.
Matandazo ni mimea hai au mabaki inayopandwa kwa madhumuni ya kufunika udongo mwaka mzima.
Kanuni ya kufunika udongo kwa mimea jamii ya mikunde, nyasi na mingineyo ndiyo muhimu zaidi na ya msingi kuliko zote.
Mizizi ya matandazo ina uwezo wa kutindua na kulainisha udongo kwa kiwango kikubwa zaidi ya majembe tunayokatulia. Kilimo cha matandazo kinaondoa ulazima wa kukatua.
KUPANDA BILA KULIMA.
Inawezekana kupanda kwenye matandazo bila kuyalima kwa kutumia zana maalum. Hizi ni pamoja na Mwuo ( Dibbler ), Jembe la mkono, Kipanzi mkono ( Jab Planter), Kipanzi komoleo matandazo ( Direct seeder ).
KANUNI ZA KILIMO HIFADHI MATANDAZO.
- Funika udongo wakati wote kwa mimea hai au mabaki yake.
- Usichome moto, usihamishe mabaki ya mazao, usichungie mifugo holela.
- Usilime/uaikatue udongo.
- Panda kwa kukomelea kwa zana maalum.
- Kilimo cha mzunguko.
Mikunde > Nyasi > Mikunde Miti > Nyasi.
HATUA ZA KILIMO HIFADHI.
1. Andaa shamba.
* Punguza uchachu wa udongo kama upo kwa Mbolea ya Minjingu, Chokaa au mmea uitwao Lupins.
* Tindua au katua kina kirefu kuondoa Mgandamano wa udongo kama upo.
* Panda Matandazo yasiyooza haraka na yenye mazap au mabaki mengi. Matandazo yanaqeza kupandwa kwa mfumo wa Kilala bora, Mchanganyiko au Kupokezana.
2. Fyeka na laza matandazo kwa Nyengo, Gogo au Kisu Kidekuzi ( Chopping knife roller ) juma 1-2 kabla ya kupanda zao kuu.
3. Pulizia dawa ya kuua wadudu ( kama ni lazima ).
4. Panda kwenye Matandazo kwa Kipanzi maalum. Weka mbolea ya asili ya kupandia.
5. Palilia magugu nachache yatakayoota kwa kung'olea au kupiga dawa ya magugu.
6. Rutubisha kwa kuongeza kiwango cha mbolea za viwandani ( kwa mwaka wa kwanza ). Dhibiti magonjwa/wadudu hasa kwa dawa za asili.
7. Kwa msimu unaofuata, rudia mzunguko kwa kilimo cha mzunguko wa mazao.
MANUFAA YA KILIMO HIFADHI.
i. Kuongeza mboji na rutuba ya udongo. Hatimaye mahitaji ya mbolea za viwandani hupungua.
ii. Kupunguza mahitaji ya nguvu kazi na muda kwa hadi 60%. Hii inatokana na kutohitajika kukatua na haro.
iii. Kuongeza kiwango cha mvua kupenya kwenye ardhi na udongo kutunza unyevunyevu. Athari za vipindi vya ukame au mvua kupita kiasi ni ndogo zaidi katika kilimo cha matandazo.
iv. Kupunguza mmomomonyoko wa udongo. Matone ya mvua hukingwa yasidondoke kwenye udongo n kuusambaratisha. Uchafuzi wa maji katika mito hupungua.
v. Kupunguza gharama za uzalishaji mazao na kuongeza faida. Baadhi ya Matandazo ( Mucuna, Marejea, Desmodium, Vetch ) yana uwezo wa kudhibiti magugu sugu kama ndago.
vi. Kupunguza uchakavu wa zana, mitambo na mafuta kwenye kilimo.
vii. Kutindua na kulainisha ardhi iliyo gandamana. Mizizi ya baadhi ya mimea ya matandazo ( Mbaazi, Fiwi, Nyonyo, Utupa, Marejea pori ) inaweza kwenda chini hadi futi nne.
CHANGAMOTO ZA KILIMO HIFADHI.
. Ni shida kuwashawishi wakulima, wataalam wa ugani, na hata watafiti kubadili mtazamo na kukubali Kilimo Hifadhi.
. Inahitaji kiwango cha juu cha nidhamu na usimamizi wa kilimo.
. Kuzuia uchungaji holela wa mifugo.
. Kuzuia utayarishaji wa mashamba kwa kuchoma moto.
. Matandazo ni makazi salama ya Panya na Nyoka.
Kwa hiyo ndugu zangu wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo, ni vema kuweza kubadili mawazo na mtazamo wa kifikra katika kuongeza kipato kwa gharama nafuu.
Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Agriculture Field Officer.