Monday, April 28, 2014

MICHAKATO YA KUHIFADHI VYAKULA MBALIMBALI KWA KUKAUSHA.

Wakulima wengi huingia hasara kubwa pale mazao yao yanapoharibika kwa kukosa masoko. Kufahamu michakato ya ukaushaji mazao utawawezesha kuyaweka katika hali ya kutoharibika na hivyo kuweza kutumiwa kwa muda mrefu. Pia ukaushaji huwezesha vyakula kutumika kwa muda mrefu bila kuharibu ladha na ubora wake.

Ukaushaji wa vyakula mbalimbali hutumiwa na wakulima wengi kama njia mojawapo ya kuepusha uharibifu wa mazao na kuviwezesha kutumika kwa muda mrefu. Yafuatayo ni maelezo ya michakato mbalimbali inayotumika kuvikausha vyakula hivyo.

MBOGA: Majani ya kunde, Matembele, Mchicha na Majani ya Maboga.

* Chambua mboga vizuri na chuma majani machanga.
* Safisha mboga vizuri
* Chemsha kwenye maji ya moto kwa dakika 1-5 (inategemeana na ugumu wa mboga, laini ni dakika chache na ngumu ni dakika nyingi) kwenye maji yenye chumvi ili rangi ya kijani iaitoke.
* Chuja kwa kutumia chekeche
* Anika nje kwenye chombo safi kama mkeka, ungo, chekeche. Epuka kukausha kwenye jua kali, anika kivulini na jua la asubuhi kabla halijawa kali.
* Kausha mpaka mjani yavunjike kwa urahisi na geuza geuza mara kwa mara.
* Weka katika chombo kinacho funika kama debe, kopo n.k.

MATUNDA: Nyanya, Ndizi, Maembe, Tende, Zabibu, Ukwaju, Nanasi.

* Tumia kisu kisichopata kutu kwa kukata matunda ili kuzuia matunda kuwa meusi.
* Osha na katakata vipande vyembamba. Ndizi ni lazima umenye.
* Tende, zabibu, ukwaju unaanika hivyo hivyo nzimanzima.
* Ndizi chemsha kwa dakika 5 katika maji ya chumvi ili kuzuia rangi mbaya isitokee.
* Kausha taratibu kwenye jua la kiasi mpaka zikauke.
* Weka katika vyombo visivyoingiza unyevu.

Kabeji

* Osha na katakata vipande vyembamba
* Chemsha kwa dakika 2 tu kwenye maji yenye chumvi.
* Chuja na anika kwebye chombo safi mpaka zikauke.
* Weka katika vyombo visivyoingiza unyevu.

Kisamvu

* Angalia majani laini na twanga.
* Chemsha katika maji yenye chumvi kidogo kwa dakika kumi ili kupunguza sumu hasa kama umechuma majani ya muhogo.
* Kausha katika chanja kwa kutumia mkeka safi, ungo au chekeche.
* Weka katika chombo kisichoingiza unyevu.

MIZIZI: Viazi vitamu na mihogo.

* Tumia viazi au mihogo iliyokomaa.
* Menya, katakata vipande vyembamba kidogo.
* Safiasha au chemsha katika maji kwa dakika tano.
* Kausha katika chanja na katika hali ya usafi.
* Ikikauka weka kwenye chombo safi kisichoingiza unyevu.

Imetayarishwa na Marcodenis E. Misungwi, mtaalam wa kilimo na mifugo.

Sunday, April 27, 2014

SABABU ZINAZOWEZA KUATHIRI CHANJO KUTOA KINGA KWA KUKU INGAWA WAMECHANJWA.

Uzoefu umeonyesha kuwa wafugaji wengi wa kuku wa kisasa (Commercial Chicken). Kuku hupatwa na magonjwa ya virusi licha ya kuwa wamechanjwa. Tatizo hili limekuwa likitokea hasa kwa ugonjwa Gumboro (Infectious Bursal Disease).

Zipo sababu ambazo kama mfugaji hakuzingatia kanuni na taratibu za uchanjaji kuku ugonjwa unaweza kutokea.

. Ratiba ya chanjo.

Kutokufuata ratiba ya utoaji chanjo (Vaccination Programme) iliyopendekezwa na mtaalam wa mifugo wa eneo au kanda husika, kunaweza kusababisha kuku wasipate uwezo wa kujikinga na ugonjwa huo ingawa watakuwa wamechanjwa. Hivyo inashauriwa kufuata ratiba ya utoaji wa chanjo iliyopendekezwa kitaalam.

. Utunzaji mbaya wa Chanjo.

Chanjo iliyohifadhiwa katika joto kali hupoteza uwezo wa kufanya kazi. Vile vile kuweka Chanjo kwenye freezer huathiri uwezo wa Chanjo husika.
Inashauriwa Chanjo kuhifadhiwa kwenye hali ya ubaridi wa joto kati ya nyuzi joto 2°C-8°C hasa kwenye friji.

Kumbuka kwamba kuna baadhi ya chanjo kwa sasa zimepigwa marufuku kusambazwa kwa kuonekana kuchakachuliwa na kupoteza ubora wake wa kutibu. Chanjo iliyozuiwa ni ya "Matone" inayozuia ugonjwa wa Kideri. Ni vema ndugu mfugaji uwe mfuatiliaji wa mambo kila wakati.

. Ugonjwa

Iwapo kuku tayari wameshapata virusi vya ugonjwa husika, wanaweza wakaugua ugonjwa huo hata kama watachanjwa chanjo ya ugonjwa huo.

Kwa hiyo basi kabla hujawachanja kuku wako wachunguze kwanza kama hawana dalili ya kuugua, lakini la muhimu kuliko yote ni kuzingatia ratiba ya uchanjaji maana yawezekana wakawa hawaonyeshi dalili ya kuugua lakini kumbe wadudu wakawa wameshaingia.

. Kutofuata masharti ya watengenezaji wa Chanjo kuhusu matumizi ya Chanjo.

Mbali na maelekezo ya matumizi ya chanjo ambayo hutolewa na wataalamu wa mifugo au wauza madawa ya mifugo wanaotambulika katika kutoa huduma hiyo. Ni muhimu pia kuzingatia masharti ya mtengenezaji chanjo husika.

. Usafirishaji na utoaji Chanjo.

Usafirishaji wa chanjo katika mazingira yasiyofaa huathiri nguvu ya Chanjo, pia utoaji wa Chanjo yenyewe na wataalam wa mifugo au madawa ya mifugo huathiri zoezi lote (Vaccination Procedure) la uchanjaji wa kuku. Inaahauriwa Chanjo isafirishwe kwenye chombo au kifaa chenye ubaridi au chenye uwezo wa kuhifadhi joto linalotakiwa, pia kuzingatia taratibu zote za mwenendo wa kuchanja kuku.

. Lishe duni.

Chakula ambacho kina viinilishe duni vinavyohitajika kukidhi afya bora ya kuku husababisha kuku kuwa dhaifu, hivyo huwa mwili wa kuku hauna uwezo wa kujikinga na magonjwa. Hivyo ni vema kulisha chakula cha kuku chenye ubora unaokidhi mahitaji ya afya ya kuku.

. Utumiaji wa dawa za tiba na chanjo kwa pamoja.

Hii pia huathiri uwezo wa Chanjo kufanya kazi kwenye mwili wa kuku. Ni vema kutowapa chanjo na dawa za tiba (antibiotics) kwa wakati mmoja. Inashauriwa kutowatibu kuku siku mbili kabla na baada ya chanjo kutolewa pia wapewe vitamini kama Vitalyte, Poultry antistress, Vitastress, Stressvita n.k.

. Vijisumu (mycotoxins).

Hivi ni vijisumu ambavyo huwa kwenye chakula cha kuku kilichohifadhiwa vibaya kama vile unyevunyevu au kwenye tandiko chafu, hivyo kuku akila chakula chenye vijisumu hivi hupunguza kinga za mwili kupambana na magonjwa, kwani vijisumu hivi hushambulia sehemu muhimu ndabi ya mwili wa kuku ambazo hujihusisha na kinga na magonjwa. Hivyo inashauriwa vyakula vya kuku vihifadhiwe kwenye sehemu isiyokuwa na unyevunyevu au joto kali, pia nafaka zinazotumika kutengeneza chakula cha kuku changanya na vitu vinavyosaudia kupambana na vijisumu hivi. Waweza kutumia Farmacid premix na mycobind kwenye chakula.

. Usumbufu (Stress)

Kuku waliopata usunbufu siku chache kabla au baada ya chanjo huwa wanapungukiwa na uwezo wa kupokea chanjo ili kujikinga na ugonjwa, usumbufu unaweza kuwa msongamano (overstocking), kukata midomo (beak trimming), kuwahamisha kuku kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hivyo epuka usumbufu kwa kuku unapokaribia muda wa kuwapa Chanjo ili kufanya chanjo ifanye kazi vizuri.

Imetayarishwa na Marcodenis E. Misungwi, Mtaalam wa Kilimo na Mifugo.

Friday, April 18, 2014

UTUNZAJI BORA WA MAZAO BAADA YA KUVUNA.

Ndugu zangu wakulima, wadau wote wa kilimo na wasomaji wa mtandao huu. Tunaelekea kwenye mavuno sasa ambapo sehemu mbalimbali ama wameanza au wako kwenye mavuno.
Katika mchakato wa uvunaji, ni kipindi cha kuwa makini sana maana unaweza ukazalisha vizuri lakini ukaja kupoteza kiasi kikubwa wakati wa mavuno.

Katika kuhakikisha kwamba mazao yanakuwa katika ubora na hali nzuri kwa mlaji (consumer), wadau katika mchakato huu lazima waunganishe nguvu za pamoja. Hebu tuwatambue wadau hawa na wajibu na majukumu yao katika mchakato huu.

(i) Mkulima
(ii) Serikali
(iii) Maafisa Ugani
(iv) Wauza Pembejeo (Stockissts)

Wajibu wa Mkulima

- Kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo.
- Kuvuna na kuandaa mazao
- Kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu.
- Kuwasilisha matatizo yao kwa wagani ili waweze kujadiliana jinsi ya kuyatatua.
- Kutumia mbinu za kienyeji zenye kuleta mafanikio.
Wajibu wa Serikali

- Kutunga na kusimamia sheria na sera (mfano sheria ya Dumuzi)
- Kuwawezesha wagani kuwasaidia wakulima (mafunzo)
- Kufanya utafiti
- Kutoa ruzuku au mikopo midogo midogo kwa ajili ya kuendeleza hifadhi ya mazao.
- Kutunga na kusimamia Sera ya Masoko.

Wajibu wa Wagani

- Kuwatembelea Wakulima na kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali na jinsi ya kuzitatua.
- Kuwaunganisha wakulima na watoa huduma mbalimbali.
- Kuunganisha wakulima na watafiti.

Wajibu wa wauza Pembejeo

- Kuwauzia wakulima Pembejeo bora ikiwa ni pamoja na viuatilifu vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaostahili
- Kutoa elimu kwa wakulima.

MAANA HALISI YA UHIFADHI NA UPOTEVU WA MAZAO.

* Uhifadhi ni kitendo cha kuweka mazao yako sehemu maalum kwa muda maalumu kabla ya kuuzwa au kutumika.

* Upotevu wa mazao ni hali ya kupungua thamani kwa mazao kutokana na sababu mbalimbali kama vile kusinyaa, kunyauka, kuliwa na wadudu, kuibiwa au kupotea.

Madhumuni ya kuhifadhi

. Kwa ajili ya chakula
. Kwa ajili ya biashara
. Kwa ajili ya biashara
. Kwa ajili ya mbegu

AINA YA UPOTEVU WA MAZAO.

Upotevu wa mazao unaweza kutokea kwa namna mbalimbali kama:

1. KUPUNGUA UZITO

Kuna aina nyingi za visababishi na vingi ni vile vinavyokula mazao hasa wadudu na wanyama kama Panya. Aidha uvunaji usio na umakini huacha mazao mengi shambani na hivyo uhifadhi kuanza na kiasi pungufu kuliko ilivyokusudiwa.

2. KUPUNGUA KWA UBORA

Visababishi vikuu ni wadudu wanaokula, wanaochafua, au shughuli inayovunja au kuharibu punje, kuchafua mazao kwa aina yoyote au kuoza, kusinyaa, kutoa harufu n.k

3. UPOTEVU WA VIINI LISHE

Visababishi vikuu ni vile vinavyokula viini vya punje ambavyo ndivyo vyenye virutubisho na vitamini. Kadhalika hifadhi duni.

4. UPOTEVU WA MAPATO

Hutokana na yote yaliyotajwa hapo juu ambapo matokeo yake ni zao kupata ndogo kwenye soko na hivyo uchumi wa mkulima kuwa duni.

5. UPOTEVU WA NGUVU YA UOTO KWENYE MBEGU.

Visababishi ni hifadhi duni na vyote vilivyotajwa hapo juu.

Katika mzunguko mzima wa uvunaji, kuna ngazi mbalimbali za upotevu ambazo ni;

- Kuvuna
- Kusafirisha
- Kukausha
- Kupukuchua/kupura
- Kupepeta/kuchambua
- Kupanga madaraja
- Kuweka dawa ya kuua wadudu
- Kuhifadhi kwenye vifaa au maghala
- Kutumia kwa chakula au kuuza
- Kusinsika.

Hebu basi tujadili sasa njia za kuweza kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvuna.

DHANA SHIRIKISHI YA UDHIBITI WA VISUMBUFU.

Aina za wadudu waharibifu:

i. Dumuzi
ii. Fukusi wa mahindi
iii. Mende mwekundu wa unga
iv. Wadudu jamii ya nondo/vipepeo
v. Visumbufu wengine ni wanyama waharibifu wakiwemo Panya.

UDHIBITI WA VISUMBUFU AINA YA WADUDU.

. Udhibiti kwa njia ya asili (Cultural control)
. Udhibiti kwa kutumia viuatilifu (Chemical control)
. Udhibiti kwa kutumia nguvu ya binadamu (Physical control)
. Udhibiti husishi (Intergrated Storage Management)

Katika udhibiti kwa njia ya viuatilifu, inatakiwa mkulima awe mwangalifu kuangalia viuatilifu sahihi na viwango vya kutumia. Kadhalika matumizi salama ya viuatilifu na tahadhari yatasisitishwa.

Mambo mengine muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika matumizi ya viuatilifu ni pamoja na;

. Kukauka kwa nafaka
. Usafi wa nafaka
. Kuchambua nafaka
. Kugawa zao
. Viwango sahihi
. Kutumia viuatilifu ambavyo havijakwisha muda wake
. Usafi na hali ya ghala au vyombo vya kuhifadhia
. Ukaguzi wa mara mara wa nafaka na ghala.

Sasa tuangalie jinsi ya ktumia viuatilifu aina ya vumbivumbi. Kabla ya kuanza shughuri nzima ya kutumia kiuatilifu (dawa), mambo muhimu ya kuzingatia ni;

(i) Kuhakikisha ni kiuatilifu kilichopendekezwa na wataalamu

(ii) Kusoma lebo na kufuata maelekezo kwa usahihi

(iii) Jinsi ya kupima na kujua kiwabgo kilachoshauriwa

(iv) Jinsi ya kuhakikisha kwamba nafaka imekauka kwa kiwango kinachostahili

(v) Kuzingatia mwelekeo wa upepo wakati wa kutumia

(vi) Jinsi ya kusafisha magunia au vyombo vingine kabla ya kuvijaza nafaka

(vii) Mambo ya kuzingatia katika kuondokana na vifungashio vilivyokwisha kiuatilifu pamoja na viuatilifu vinavyobaki.

(viii) Tahadhari za kiafya wakati wa kutumia viuatilifu.

Jinsi ya kutumia viuatilifu aina ya majimaji kutayarisha ghala.

Zoezi hili litazingatia mambo yafuatayo ;

(i) Tofautisha matumizi ya viuatilifu vya majimaji na vile vya vumbivumbi katika hifadhi.

(ii) Jinsi ya kuchanganya kiuatilifu cha majimaji kupata kiwango kinachostahili.

(iii) Matumizi sahihi ya mabomba ya kunyunyizia viuatilifu.

Njia mbadala kwa madawa ni kutumia vifaa visivyoingiza hewa kama vile mapipa.

Udhibiti wa Panya

Panya ni visumbufu katika kundi la wanyama, hushambulia zaidi mazao ya nafaka kuanzia shambani hadi ghalani na hupunguza kipato cha mkulima kwa kiwango kikubwa asipo dhibitiwa. Ili kuweza kumdhibiti Panya ni lazima;
- Ujue tabia za Panya

- Ujue jinsi ya kutambua maeneo wanakopita.

- Ujue sumu za Panya (sumu za kizazi cha kwanza na za kizazi cha pili).

Ujue namna sahihi ya utegaji wa Panya.

Note: aina hizo za dawa yaani kizazi cha kwanza na kizazi cha pili, kizazi cha kwanza ni dawa ambayo inaua Panya peke yake na kizazi cha pili ni ile dawa ambayo inaua mtambuka pale ambapo kuku akimdonoa Panya aliye kufa, na huyo Kuku atakufa kutokana na hiyo dawa. Zipo hadi kizazi cha tatu ingawa ni mara chache ambapo binadamu au mbwa akimula huyo Kuku, atakufa.

Kwa hiyo ndugu zangu wakulima na wote mnaotembelea kwenye blog hii, tujitahidi kadri tuwezavyo kukabiliana n upotevu huu.

Sunday, April 13, 2014

ZIARA YA KAMATI YA UCHUMI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBOZI YATEMBELEA MRADI WA BWAWA LA NANSAMA.

Jopo la waheshimiwa madiwani, Kamati ya Uchumi wametembelea mradi wa maji kwa ajili ya huduma za umwagiliaji katika kijiji cha Nansama kata ya Isansa.

Mradi huu ulianzishwa kwa uwezeshwaji kama kikundi cha kahawa Igabda na benki ya NMB chini ya kitengo chao cha Development Foundation ukigharimu Tsh. 30,000,000/= hata hivyo baada ya ujenzi kumalizika na watu kuanza kutumia, lilibomoka na halmashauri kupitia Idara ya Kilimo iligharamia ukarabati huo. Na tokea hapo mradi sasa uko chini ya halmashauri.

Kamati iliongozana na jopo la watumishi kutoka katika Idara mbalimbali hasa zinazoshabihiana na Kilimo wakiongozana na Mkaguzi wa ndani.

Kamati ilimuomba mwenyekiti wa bwawa atoe maelezo ni historia fupi juu ya jinsi mradi ulivyoanzishwa na unufaika wa wananchi katika mradi huo. Mwenyekiti alieleza kwa kifupi na kukumbushia ushauri uliokwishatolewa na mkuu wa mkoa pindi alipotembelea mradi h mwezi January wa halmashauri kuweza kuangalia uwezekano wa kulipanua zaidi ambapo sambambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa alishauri miti ipandwe kulizunguka bwawa ambalo hilo l miti limekwisha tekelezwa na miti imepandwa na inaendelea vizuri. Maswali mawili matatu pamoja na ushauri yakaulizwa.

Bi. Lydia Shonyela, ambaye alimwakilisha Afisa Kilimo na Umwagiliaji (DAICO) pia alitoa baadhi ya maelezo ya jinsi halmashauri ilivyosaidia katika mradi huo.

Baada ya hapo waliondoka kuelekea kata Ruanda.