Friday, March 28, 2014

UZALISHAJI WA MBEGU BORA ZA MAHARAGE - DARAJA LA KUAZIMIWA UBORA (Quality Declared Seed), QDS.

Maharage n zao muhimu kwa chakula, lishe na kipato kwa familia na Taifa. Kwa mavuno mengi ni vizuri kuzingatia kanuni bora muhimu za kilimo bora cha Maharage. Mavuno mengi na yenye ubora huchangiwa na matumizi ya mbegu bora. Mbegu bora ni mojawapo ya pembejeo muhimu katika Kilimo. Ubora wa mbegu unatakiwa kufuata hatua zote za uzalishaji mbegu shambani, uvunaji, usafirishaji, kupakia kwenye vifaa, kufunga, usambazaji, kuhifadhi na uuzaji.

Mbegu ya kuazimiwa ubora (quality declared seed) huzalishwa na wakulima wadogo wadogo na vikundi vya wakulima wadogo vijijini, chini ya usimamizi wa washauri wa Kilimo wa Wilaya.

SIFA ZA MBEGU BORA/VIPIMO VYA UBORA WA MBEGU.

. Mbegu za aina moja (uhalisia wa kizazi) - Ili kuwa na sifa hii ukaguzi lazima uanzie kwenye shamba la kuzalisha mbegu.

. Mbegu safi - Zisizochanganyika na aina zingine au mazao mengine, mbegu za magugu, zisizoliwa na wadudu na uchafu kama udongo na takataka zingine.

. Mbegu zilizokomaa na kukauka vizuri - Kama zimekauka vizuri haziwezi kuoza na kuvunda, na huota vizuri pia haziwezi kushambuliwa na wadudu kwa urahisi. Hii huiwezesha mbegu ibaki na ubora wake kwa muda mrefu.

. Mbegu zilizovunwa kutoka mimea yenye afya kutoka shamba lenye mazao mazuri - Mbegu zilizovunwa kutoka kwenye mimea dhaifu haziwezi kuota vizuri na kwa wakati mmoja na mimea yake huwa dhaifu.

. Mbegu yenye afya nzuri - Mbegu ambayo haiwezi kuwa chanzo cha magonjwa. Fungu la mbegu isiyo salama kiafya isitumike kama mbegu. Vime vya magonjwa huweza kusambazwa kwa njia ya mbegu kama mbegu hii itatumika.

. Mbegu zenye uwezo wa kuota kwa zaidi ya asilimia tisini (90%).

. Mbegu za aina bora zinazokibalika (chagua aina ya mbegu kulingana na mahitaji).

. Mbegu mpya (pre-basic/foundation), isirudiwe kupandwa zaidi ya misimu miwili.

SEHEMU YA KUPANDA.

. Panda sehemu zenye udongo usiotuamisha maji na wenye rutuba.

. Panda mbegu katika maeneo yenye mwinuko wa mita 400m-1800m kutoka usawa wa bahari kwa nyanda za juu kusini.

WAKATI WA KUPANDA.

. Usipande kipindi cha mvua nyingi zinazoanza mwezi Novemba au Disemba hadi April au mei, panda mwezi Februari hadi March.

. Sehemu kavu zenye mvua ya muda mfupi kama, panda mwezi Disemba hadi Februari.

. Sehemu zenye maji ya umwagiliaji panda wakati wa kiangazi.

UPANDAJI.

. Panda kwa nafasi zinazoshauriwa sentimita 50 mstari hadi mstari na sentimita 10 mbegu hadi mbegu (50cm × 10cm).

. Tenga aina mbalimbali za mbegu kwa nafasi ya mita zisizopungua mita 3.

. Usipande mbegu katika mchanganyiko wa mazao mengine.

MBOLEA

. Weka mbolea wakati wa kupanda kama inavyopendekezwa. Mfano, mifuko 1 (kilo 50) TSP na 3/4 (kilo 40) mfuko CAN au DAP mfuko 1 (kilo 50).

PALIZI

Wahi palizi ya kwanza ndani ya wiki 2 baada ya maharage kuota na rudia tena kabla ya kuchanua. Unaweza kutumia madawa ya kuua magugu kama SATECA au Stomp.

WADUDU

. Funza wa maharage ni wadudu wanaoshambulia mimea michanga ya maharage. Funza wa maharage hawa huweza kusababisha uharibifu hadi kufikia asilimia 100 kufuatana na hali ya hewa-unyevu kidogo, rutuba kidogo, kuwepo kwa maotea ya aina ya maharage na magonjwa kwenye udongo, kurudia kupanda zao la maharage kila msimu na aina ya naharage.

Njia nzuri ya kudhibiti funza wa maharage haws ni:-

1. Kupanda mapema

2. Kupakaza mbegu dawa kama endosufan, Acephate, Murtano (mchanganyiko wa dawa ya fungas na wadudu) nasaidia kuzuia funza wa maharage na visababishi vya kuozesha mizizi.

TAHADHALI: Dawa ya Murtano ni sumu kali hivyo mbegu zenye dawa hii zisitumike kwa chakula.

3. Kunyunyizia dawa mfano Karate 5EC au Actellic 50EC ndani ya siku 4 hadi 5 baada ya maharage kuota.

4. Kupanda mbegu zenye afya kwenye udongo wenye rutuba.

5. Kupanda mbegu zenye ukinzani wa funza wa maharage.

6. Kuweka matandazo kama pumba ya mpunga husaidia kuotesha mizizi mipya n kurudisha afya ya mmea wa maharage.

MAGONJWA

Magonjwa maarufu ni ndui ya maharage, madoa pembe, kutu, magonjwa yanayosababishwa na bacteria na virusi. Mbegu iliyoambukizwa, udongo na takataka za maharage ni vyanzo vikubwa vya uambukizaji kwa magonjwa yote isipokuwa ugonjwa wa kutu ya majani.

1. Punguza athari kwa kupanda mbegu safi, zenye afya zisizo na vidonda/ magonjwa, aina zinazovumilia na kutunza shamba.

2. Panda kwa mzunguko wa mazao ya jamii nyingine.

3. Ondoa na kuchoma yaliyougua.

4. Tumia dawa zilizopendekezwa kama Kocide, Funguran, Bayleton n.k kwa kuzuia magonjwa yanayosababishwa na ukungu na bacteria.

KUVUNA NA KUTAYARISHA MBEGU.

Vuna maharage mar yatakapokauka. Kausha kwa kuanika juani, piga, peta na kausha tena juani. Unaweza kuvuna kilo 600 hadi 800 kwa ekari kabla ya kuchambua endapo utafuata kanuni za kilimo bora.

Chambua mbegu vizuri kwa kuondoa uchafu, udongo, mbegu za aina nyingine, punje zilizopasuka na zilizohafifu. Pia ondoa punje zenye vidonda/mabaka na zilizotobolewa na wadudu. Hakikisha mbegu zimekauka vizuri kabla ya kuhifadhi.

KUHIFADHI MBEGU.

Safisha vyombo au ghala na ondoa wadudu. Zuia wadudu kwa kutumia dawa za asili au za viwandani. Tumia dawa za kuhifadhia mbegu kama Actellic (gramu 100 za Actellic super Dust kwa kilo za mbegu za maharage), Murtano (gramu 300 za Murtano kwa kilo 100 za mbegu za maharage) na dawa zinginezo kwa kiwango kinachoshauriwa na wataalamu. Weka mbegu mbali na maharage ya chakula pamoja na vyakula vingine. Epuka sehemu zenye unyevu na paa zinazovuja na zuia panya. Usihifadhi mbegu kwa zaidi ya misimu miwili maana baada ya hapo uwezo wa kuota hupungua.

KUPIMA UWEZO WA KUOTA

Pima uwezo wa uotaji kabla ya kupanda. Uotaji mzuri ni wa zaidi ya asilimia tisini (90%).

Panda mbegu 100 katika kila sehemu tatu zinazofanana na zenye unyevu. Baada ya siku kumi chunguza miche iliyoota vizuri na kuihesabu.

Tumia kanuni ifuatayo:-

Asilimia ya uotaji = miche iliyoota vizuri × 100 gawanya kwa 300.

Ahsanteni sana!

Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Agriculture Field Extension Officer III, Mbozi District Council, Mbeya.

Friday, March 21, 2014

KILIMO CHA UYOGA.

Ndugu zangu wakulima, wadau wa kilimo na watembeleaji wa blogu hii, kama mnakumbuka nilishawahi kuandika kuhusu mada hii ya Uyoga. Leo ntaelezea kwa kina zaidi kuhusu kilimo hiki cha Uyoga hasa kwa lengo la kuufahamu zaidi.

UTANGULIZI.

Uyoga ni aina ya nyuzi kuvu (fungus) yenye kutofautiana na mimea mingine kwa kukosa chembe chembe zinazowezesha mimea kujitengenezea chakula yenyewe kwa kutumia hewa na mwanga.

Uyoga unaota wenyewe kwenye mashamba hasa wakati wa mvua kwenye maeneo yenye mboji nyingi. Sasa hivi nchini tunao utaalamu wa kuotesha uyoga au ndani ya nyumba au nje kwenye kivuli maalumu.

HISTORIA FUPI YA UYOGA.

Uyoga umefahamika na wanadamu tangu enzi za zamani sana. Miaka elfu nne kabla ya kuzaliwa Kristo watu walijua uyoga. Historia inatueleza kwamba watu wameanza kulima kwa utaalamu mwaka 300 baada ya kuzaliwa Kristo.

Wadadisi wa mambo wanauelezea Uyoga kufanana sana na chakula waisraeli walichokuwa wakila kule jangwani katika safari yao ya kutoka utumwani Misri.

Wakati Uyoga ukilimwa katika dunia yote, hapa Afrika na hasa kwetu Tanzania mambo yalikuwa ni tofauti kabisa. Hakuna mtu aliyesumbuka na kilimo hicho. Ni hapo majuzi tu mwaka 1993 ndipo ukulima ulianza Dar es salaam. Mwaka 1994 ukulima ulianza Arusha, mwaka 1995 ukulima ulianza huko Mbeya, na mwaka 2003 ukulima ulianza huko Kilimanjaro.

AINA YA UYOGA.

Inakadiriwa kuwa kuna aina milioni moja na laki tano (1,500,000) za nyuzi kuvu (fungus) duniani; katika hizi ni aina 64,000 ambazo zimekwisha kufanyiwa utafiti na kupatiwa maelezo ya kisayansi. Katika hizi aina 64,000, kuna ambazo zimethibitika kuwa na Uyoga halali 12,000. Na kati ya hizi ni aina 2,000 na ndizo zinazolimwa.
Katika aina 2,000 za uyoga zilizokwisha thtbitika, hapa Tanzania ni aina 40 tu.

Uyoga Mamama (Oyster mushroom).

Aina hii ya Uyoga hustawi katika nchi za Tropics. Utaalamu unaohitajika siyo mgumu. Baadhi ya aina zinazooteshwa ni hizi zifuatazo;
. Pleurotus oystreotus
. Pleaurotus sajo-caju
. Pleaurotus sapidus
. Pleurotus flabel atus - (pink oyster)
. Leaurotus Pulmonerius
. H. K. n.k
. Monkey Head
. Auriclaria

Nyingine zinazooteshwa hapa nchini kwa kiasi kidogo ni;
. Agaricus bitoquis (uyoga vifungu)

Uyoga taka ambazo ni;
. Coprinus cinereus
. Caprinus Comatus
. Lentinus edodes
. Volvoriella Volvocea

Nyingine ni;
. Ganodema lucidum

FAIDA ZA UYOGA

Uyoga una maajabu makubwa katika maisha ya mwanadamu, Uyoga ni lishe bora kwa mwanadamu, ni dawa na tiba kwa mwanadamu, ni zao la kuingizia watu kipato, ni rafiki wa mazingira pia.

LISHE

. Uyoga ni zao lenye viini lishe (amino acids) zote 22 zinazohitajika na mwili wa mwanadamu.

. Protini iliyoko kwenye Uyoga inafikia kiwango cha asilimia arobaini. Hii inalingana na protini iliyoko kwenye maziwa.

. Kuna wingi mkubwa sana wa vitamini B,C na D.

. Uyoga hauna mafuta mengi. Una asilimia tatu tu. Hivyo hauna Colestrol.

. Uyoga unayo madini yote muhimu kwa mwanadamu; phosphorus, Iron, Calcium na Potash.

TIBA

Utafiti uliofanyika siku za karibuni umethibitisha kuwepo kwa dawa nyingi ndani ya uyoga zenye uwezo wa kutibu kwa ufanisi, magonjwa ya wanadamu na mifugo. Kwa wanadamu magonjwa yafuatayo yanatibiwa;

. Kifua kikuu TB
. HIV/AID upungufu wa kinga mwilini
. Kisukari
. Shinikizo la damu
. Magonjwa ya moyo na uti wa mgongo
. Saratani
. Matatizo ya figo
. Vifo vya watoto wachanga

AJIRA

Kwa sasa hivi ajira imepungua sana katika nchi yetu. Vijana, wazee na rika lote hatuna kazi, mazao yaliyokuwa yakituingizia kipato yamepungua au yamekwisha. Nguvu kazi nyingi tuliyonayo inatumika kuuza mwanasesere na plastic zinazotoka katika nchi za nje.

Watu wengi mno tunaishi katika lindi la ufukara. Hatuna mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi na mavazi bora. Kufuatana na ripoti ya umoja wa mataifa, iliyoandaliwa na Professors S. T. Chang na Mshigeni wa chuo kikuu cha Namibia, mauzo ya Kahawa kwenye soko la ulimwengu kwa mwaka 1997 ni dola za kimarekani bilioni 15. Mauzo ya Uyoga yalikuwa dola bilioni 14. Katika biashara hiyo Afrika ilichangia kwa asilimia 0.3 tu.

Wataalamu hawa wanaainisha sababu nyingi zinazosababisha upungufu huu. Kubwa wanalosema ni kuwa waafrika hawajui umihimu wa uyoga katika maisha ya mwanadamu. Bei ya uyoga huko Marekani, Mashariki ya kati na Mashariki ya Mbali ni kati ya dola za Marekani tisa ($9) hadi kumi na tatu ($13). Uyoga ni zao lililo kayika mpango nafuu wa biashara ya Marekani na Afrika. Halitozwi ushuru kuingia katika masoko ya Marekani.

KUSAFISHA MAZINGIRA

Kufuatana na ripoti ya wataalamu wa chuo kikuu Kivais na Magingo ya miaka ya tisini, Tanzania inayo masalio ya kilimo na misitu zaidi ya tani milioni kumi na saba (17,000,000). Masalio haya yameachwa yakioza, au kuchomwa moto au kulishwa mchwa pamoja na mapanya. Ikiwa masalio haya yatatumika kuoteshea Uyoga, Mazingira yataboreka na uchumi utakua. Uzalishaji wa Uyoga unaanzia pale mkulima au mtumiaji wa bidhaa za kilimo na misitu anapomalizia.

MASALIO YA TAKATAKA BAADA YA KUOTESHA UYOGA.

Masalio ya takataka (vimeng'enywe) hutumika kama ifuatavyo;

. KULISHA MIFUGO

Uyoga una uwezo wa kuvunja vunja chembe chembe za vimeng'enywe na kuviboresha kuwa protini na madini mengi, kisha kufyonza hicho na kutengeneza matunda ya uyoga. Baada ya kuvuna uyoga chembechembe hizi bado zina ubora mkubwa wa chakula kwa ajili ya mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi, nguruwe, sungura n.k. Tunao wafugaji wanaotumia vimeng'enywe hivi kulishia mifugo nao wameendelea kupata maziwa mengi.

. MBOLEA

Vimeng'enywe hivi hutumika kama mbolea shambani na katika bustani. Matokeo ya kutumia vimeng'enywe hivi yameonyesha ufanisi mkubwa.

.METHANE GAS

Tukijenga mfumo wa kutengeneza gesi kama kawaida, tunaweza kutumia vimeng'enywe hivi kutengeneza methane gas. Hii gesi itatumika kupikia, kuwasha taa na mambo mengine kama hayo. Mabaki katika zoezi hili huwa na mbolea nzuri ifaayo sana. Mazao ya shamba na bustani yaliyokuzwa kwa mbolea hii yana bei nzuri zaidi sokoni, maana yanahesabika yamezalishwa kiasili (organic agriculture).

. ZERI ( Zero Emmission Research Initiative).

Umoja wa Mataiga umeiteua Tanzania pamoja na nchi nyingine katika bara la Afrika kuendeleza na kutekeleza mfumo wa ZERI. Huu ni mfumo wa kutochafua mazingira kwa njia ya kutoa moshi. Masalia ya kilimo ba misitu yasichomwe moto bali yageuzwe kutoka hali yake na kuwa kitu kingine labda kilicho bora na chenye thamani zaidi. Masalia ya sokoni hatutayaacha yaoze bure, tutayasindika ili yaweze kuzalishia uyoga. Pumba za mpunga na kahawa hatutazichoma moto. Tutazitumia kwa kuzitengenezea chipboards, vivyo hivyo na maranda ya mbao, takataka za katani, kahawa na n.k. zitageuzwa kuwa kitu bora zaidi.

UTAYARISHAJI WA SHAMBA LA UYOGA.

Mambo ya muhimu ya kuzingatia:
. Ukubwa wa shamba
. Uwezekano wa upanuzi
. Usafi wa eneo
. Upatikanaji wa takataka za kulimia yaani vimeng'enywe
. Upatikanaji wa maji safi
. Umbali kutoka kwenye soko

Ndani ya ndani

. Hewa safi ya inayozunguka
. Joto linalotakiwa
. Unyevunyevu kwenye hewa unaotakiwa
. Carbondioxide na mwanga vinatakiwa

Shamba

Shamba la uyoga linapaswa liwe na viambatanisho vifuatavyo;
. Sehemu ya kutayarisha vimeng'enywe
. Kichanja cha kuhifadhi majani au aina yoyote nyingine ya vimeng'enywe.
. Sehemu ya kuchemshia vimeng'enywe
. Sehemu ya kupandia mbegu kwenye vimeng'enywe vilivyokwisha kuchemshwa.
. Banda kamili la kukuzia lenye sifa zilizokwisha ainishwa hapo juu
. Sehemu ya kuhifadhia uyoga uliovunwa au chumba cha baridi kutegemea na hali halisi.

UJENZI WA SHAMBA

Mkulima anashauriwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika eneo lenyewe. Kwa mfano mkulima mwenye shamba la migomba, baai atumie marawa katika kuta na paa. Unaweza ukatumia nyasi za kawaida au majani ya mpunga, ngano na mengine ya namna hiyo, unaweza kutumia matofali mabichi, unaweza kutumia mabanzi. Ndani ya nyumba weka weupe. Hii ni chokaa au kitambaa cheupe. Hii ni kwa sababu uyoga hukua kuelekea rangi ya mazingira yaliyouzunguka. Lakini rangi nyeupe huchochea ukuaji na hudumisha usafi. Nyumba ya uyoga iwe na madirisha makubwa mazuri.

MAANDALIZI YA VIMENG'ENYWE

Kama ilivyosemwa hapo mwanzo, kila jani lililokomaa na kukauka, lafaa kuoteshea uyoga. Michanganyiko ifuatayo yafaa sana kuoteshea uyoga.

. Majani ya mpunga au migomba yenye unyevu 62%
. Pumba za mahindi unyevu 62%
. Sukari
. Chokaa

Vimeng'enywe viko vingi, mkulima anashauriwa awaone wataalamu kwa ushauri.

MAHITAJI MENGINE

Ifuatayo ni orodha ya mahitaji mengine;
. Jiko la kuchemshia
. Pipa tupu la lita mia mbili
. Mifuko ya plastic size 10" × 15" yenye uwezo wa kuhimili joto
. Viroba (polysacks) pvs ya kuweka ndani ya pipa
. Vibangili vya kipenyo cha 1.5
. Kamba au uzi wa kushonea viatu ili kufunga mifuko wakati wa kuchemsha.
. Vipande vya magazeti
. Rubber band size ya mpira wa ndana ya tairi ya baiskeli.

HATUA ZA KUFUATA KATIKA KUOTESHA

. Katakata majani yaliyokomaa na makavu katika urefu usiozidi nchi nne
. Changanya majani haya na virutubisho hapo juu i.e. pumba za mahindi, sukari na chokaa.
. Changanya sawasawa kwa kutumia maji safi ndoo tatu hadi tano.
. Zilundike mahali safi ukitengeneza mlinduko wenye kimo cha mita moja hadi mita moja na nusu.
. Funika kwa polythene paper na vitambaa vya sulphate
. Majani ya migomba yalowekwe kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuvundikwa
. Ziache kwa muda wa masaa 24
. Weka vimeng'enywe hivi katika mifuko ya polythene
. Weka maji lita 40 katika pipa lenye kichanja cha mbao chenye kuzuia mifuko isigusane na maji
. Bandika kwenye jiko hadi mvuke unapotoka , hesabu msaa manne.
. Ipua mifuko yako na iweke mahali safi
. Sasa ni wakati wa kufanya kila kitu kwa hali usafi. Tunatumia maji yenye detol kusuzia mikono yetu
. Otesha uyoga kama mtaalamu atakavyokuonyesha
. Baada ya siku 21 ondoa vipande vya gazeti ulivyotumia kufunika mifuko
. Baada ya siku 10 nyingine utaanza kuvuna uyoga. Uta una kwa muda wa miezi 2 hadi 3
. Weka uyoga uliovuna ili kuhifadhi ubora wa uyoga.

MAPATO YA MKULIMA

Tunaorodhesha hapa hali halisi ya mkulima wetu mwenye banda la mita tatu (3) kwa mita tano (5).

Gharama:

Majani ya mpunga Pickup moja = 25,000/-
Mifuko ya plastic 500@50 = 25,000/-
Mbegu za uyoga chupa 100@1500 = 150,000/-
Jumla = 200,000/-


Mavuno aliyopata kilo 300@3000 = 900,000/-
Toa gharama = 200,000/-
Salio = 700,000/-

Kazi hii ilimchukua mkulima huyu miezi mitatu. Ijulikane kuwa baada ya kuotesha mkulima anakagua banda kw muda mfupi sana, asubuhi saa sita na jioni. Mkulima huyu na familia yake anajipatia wastani wa shilingi 230,000/- kila mwezi kwa kulima banda moja.

MAPISHI

Mkulima na umma wote wanapashwa kujua mapishi ya uyoga.
Tunaweza kutumia uyoga kama ifuatavyo;

. Kutengeneza supu
. Kutengeneza supu ya viungo (mushroom curry)
. Kutengeneza mboga ya kawaida tunayoweza kula na vyakula vingine kama vile ugali ndizi, wali, viazi n.k.
. Tunaweza kuzindika a kutengeneza mushroom pickle (hii tutauza kwenye supermarket na mahoteli ya kawaida hasa ya kitalii)
. Tunaweza kutengeneza mushroom pizza.

MAGONJWA YA UYOGA

Uyoga ni viumbe hai. Hivyo hupatwa na magonjwa kama hali ya mazingira na utendaji haitakidhi. Kuna magonjwa ya aina kama ifutavyo;

. Bacteria

Uyoga unakuwa na rangi ya kutu. Hata mifuniko inakuwa na rangi hiyo. Ugonjwa huu unatambulika kiurahisi., kwani unakuwa unateleza.

. Fungus

Aina zifuatazo ndizo hasa zishajulikana;
. Blue mould
. Black mould
. Brown mould

. Virus

Uyoga uliopendeza unasinyaa mara moja. Unaanza kutoka jasho.

MASOKO

Mpaka sasa hoteli za kitalii zinapika uyoga wa kutoka nje uliowekwa kwenye makopo.
Ikumbukwe kuwa kwenye makopo kuna uyoga halisi kidogo sana. Pia katika supermarket za hapa nchini kuna uyoga fresh kutoka Kenya. Pia tujue kuwa majirani wetu waliotuzunguka Kenya, Uganda, Zambia na Malawi wamepiga hatua kubwa katika kilimo cha uyoga. Swali tunalopaswa tujiulize sote ni hili " Kulikoni Tanzania kuhusu Uyoga".

Tumeziona faida za uyoga. Ni bora kuliko nyama nyekundu na nyama nyeupe. Kwenye maduka ya nyama zinauzwa kilo nyingi za nyama kila siku. Badala yake tuuze uyoga kila siku.

SOKO LA NJE

Kama ilivyoelekezwa hapo juu kuna masoko ya nje. Lakini yanataka kiasi kikubwa cha uyoga. Tani kadhaa kila wiki na kila mwezi. Ili kuweza kukidhi haja hii, wakulima waunde vikundi na vyama vya ushirika ili kushughurikia jambo hili.

HITIMISHO

Andiko hili dogo lina lengo la kumuandaa Mtanzania wa kawaida aweze kuwa mkulima wa uyoga. Kamwe lisichukuliwe kama mamlaka tosha kuhusu uyoga. Sababu ni kwamba nimechagua kuzungumzia yale mepesi tu yanayoweza kumfaa mkulima wa ngazi ya mwanzo. Sayansi ya uyoga ni pana, ndefu na yenye kina.

Ahsanteni sana.

Imeandaliwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi,
Mtaalamu wa Kilimo na Mifugo III, Mbozi District Council
Kwa msaada wa International Fund for Agricultural Development, IFAD.

Monday, March 10, 2014

MAGONJWA SUGU KWA KILIMO CHA KAHAWA NA UDHIBITI WAKE

Kahawa ni zao kubwa la biashara linaloliingizia taifa fedha nyingi za kigeni. Ni la pili baada ya Tumbaku. Lakini zao hili linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni magonjwa na wadudu achilia mbali Pembejeo, haya yote yanamuhusisha moja kwa moja mkulima. Makala yangu iliyopita nilijadili kwa kina Wadudu wasumbufu kwenye kahawa na jinsi ya kujaniliana nao.

Leo nitaongelea magonjwa sugu ya kahawa na udhibiti wake.

1. CHULEBUNI (CBD).

Chulebuni ama kama ujulikanavyo kama Coffee Berry Disease (CBD), ni ugonjwa mbaya sana na huenea kwa kasi. Mbuni ulioshambuliwa haufi ila mkulima anaweza kupoteza mpaka asilimia 90 ya mavuno kama hatazingatia namna bora ya kuuzuia. CBD huathiri matunda ya kahawa hasa kanda za juu na kati. Ushambuliaji ni mkubwa zaidi wakati wa masika kwani CBD hupenda hali ya unyevu na hali ya baridi.

Dalili na madhara ya CBD:

* CBD hushambulia mibuni katika hatua tatu muhimu ambazo ni:
. Maua yanapochanua.
. Punje zikiwa changa na laini.
. Punje zinazoiva.

* Madhara makubwa hutokea walati punje zikiwa changa na laini amnapo:
. Maua yaliyoshambuliwa hunyauka na kuanguka.
. Vidonda vyeusi na vilivyobonyea huonekana kwenye matunda yaliyoshambuliwa. Mengi huoza na kudondoka. Yaliyobakia hukaukia kwenye mti na kuwa chanzo cha uambukizaji kwenye mavuno ya msimu unaofuata.

* Matunda yaliyoiva hukaukia kwenye matawi na huvunwa kama buni.

* Hupunguza zao kwa asilimia kati ya 30 na asilimia 60 wakati mwingine hufikia hadi asilimia 90.

* Kudhibiti CBD hufikia hadi asilimia 35 ya gharama za uzalishaji.

* Hupunguza ubora wa kahawa kwa kiasi kikubwa.

Jinsi ya kuzuia chulebuni (CBD):
- Panda aina mpya ya kahawa inayohimili mahambulizi ya Chulebuni ambayo ni mkombozi dhidi ya ugonjwa huu hatari.
- Punguza kivuli shambani.
-Kata matawi kwa wakati na sahihi. Ondoa maotea mara kwa mara.
- Ondoa masalia ya buni zilizoathirika na teketeza kwa moto.
- Kwangua magamba kwenye mashina machafu ya kahawa.
- Anza kunyunyizia vizuia kuvu kukinga matunda machanga ndani ya wiki tatu kabla ya mvua za msimu kuanza.
- Hamasisha majirani kuzuia chulebuni kwa wakati mmoja.

2. KUTU YA MAJANI (LEAF RUST).

Kutu ya majani ni ugonjwa unaoathiri majani ya kahawa hasa kanda za chini na kati. Ugonjwa huu unaathiri kahawa aina zote; Robusta na Arabika. Kutu ya mjani isipodhibitiwa inaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60.

Dalili za ugonjwa:

Majani yaliyoshambuliwa hutokeza madoa madoa ya manjano chini ya jani

Madhara yake:
. Kutu ya majani hupunguza eneo la jani la kutengeneza chakula. Pia hudababisha kupukutika kwa majani yanayolisha matunda na kukuza mmea.
. Kwa hali hiyo husababisha madhara ya mmea kutoa punje ndogo zenye ubora hafifu.
. Ugonjwa ukishamiri hukausha matawi, shina zima na hatimaye mti mzima kufa.

Hali zinazochangia kuenea kwa kutu ya majani:
- Unyevu wa hewani unapokuwa zaidi ya aslimia 80 na unapoambatana na kivuli cha kupita kiasi kwenye shamba.
- Msongamano wa machipukizi na matawi katika mti wa kahawa.

Jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa kutu ya majani:
- Punguza kivuli kuzunguka mti wa kahawa.
- Pogolea machipukizi na matawi katika mti wa kahawa.

Kuzuia kutu ya majani:
i) Panda aina mpya zinazovumilia magonjwa ya kutu ya majani na chulebuni.
ii) Boresha huduma muhimu ikiwa ni pamoja na lishe ili kuongeza uvumilivu wa magonjwa hususani ugonjwa wa kutu ya majani.
iii) Tumia viua kuvu kwa wakati na vipimo sahihi. Unyunyiziaji wa kwanza ufanywe ndani ya wiki tatu kabla ya mvua kunyesha, na kuendelea hadi mara tatu mpaka nne kwa msimu.
iv) Shirikisha na majirani kudhibiti kutu ya majani.

MAGONJWA MENGINE YA KAHAWA.

Yapo magonjwa mengine kadhaa ya kahawa ambayo umuhimu wake umemezwa na magonjwa mawili niliyozungumzia hapo juu. Ningependa kuyataja tu baadhi yake pamoja na mbinu za kuyazuia au kuyatibu.

3. BAKAJANI (Brown eye spot).

Ugonjwa huu huenezwa na kimelea aitwaye "Cercospora cofficola". Hudhibitiwa kwa utunzaji bora wa shamba na kutumia morututu.

4. UGONJWA WA PUNJE ( Bean disease).

Huu huambukizwa na kuvu aitwaye "Nematospora coryli" akienezwa na kimatira. Ili kuepukana na ugonjwa huu, ni lazima kuchukua hatua za kumdhibiti kimatira.

5. UGONJWA WA MASHINA (Scarly bark disease).

Ugonjwa huu hujulikana kama "Ukungu" kwa wakulima walio wengi, upo wa aina mbili ambao wakulima huwa wanashindwa kutofautisha na huuita kwa ujumla wake Ukungu. Aina hii ya kwanza ya ukungu huambukizwa na kuvu aitwaye "Fusarium lateritium". Hakuna udhibiti wa kitaalam mpaka sasa ila kung'oa mti mzima na kupanda upya. Ukishang'oa choma mti hapohapo na acha kwa muda angalau hata misimu miwili au mitatu kisha panda upya.

6. UGONJWA WA KUOZA MIZIZI (Root rot disease).

Huu ugonjwa unafanana kabisa na ugonjwa wa mashina, ni ukungu wa aina ya pili kama unavyojulikana na wakulima wengi. Huambukizwa na kuvu aitwaye "Armillaria mellea". Hakuna udhibiti ila kung'oa na kupanda upya baada ya muda wa misimu miwili au mitatu hivi.

Ndugu zangu wakulima, wataalam na wadau wote wa kilimo, hakikisheni mnajitahidi kwa kadri inavyowezekana kudhibiti magonjwa hayo. Kwa kufanya hivyo kutanuongezea mkulima kipato chake na pato la taifa kwa ujumla.

Ahsanteni sana!

Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi, Agriculture Field Extension Officer.

Sunday, March 9, 2014

WADUDU WAHARIBIFU WA KAHAWA NA JINSI YA KUWADHIBITI

Udhibiti sahihi wa visumbufu vya mimea ni njia ni njia mojawapo ya kuongeza tija katika kilimo, na ubora wa mazao. Kwa kuwa kwa kipindi hiki kuna aina za mbegu chotara nyingi za kahawa hasa zinazozalishwa na TaCRI zenye uvumilivu wa magonjwa sugu ya Chulebuni,CBD, na Kutu ya mjani. Mbegu hizi zinazaa sana na zina muonjo mzuri, changamoto kubwa imebaki kwenye udhibiti wa wadudu waharibifu. Hapa chini nitaelezea baadhi ya wadudu hao na jinsi ya kuwadhibiti.

1. KIMATIRA

Kimatira ni mdudu anayeshambulia kahawa aina ya Arabika. Madhara ya mdudu huyu ni kupunguza wingi wa na ubora wa kahawa. Wastani wa vimatira wawili au watatu kwa mti kwa eneo wanaweza kusababisha uharibifu wa zao kwa asilimia 45. Hufyonza matunda machanga na kusababisha kuoza. Hufyonza majani na machipukizi na kusababisha utoaji wa matawi madogo madogo na pingili fupi fupi. Dalili hizi zikionekana mkulima achunguze kuwepo kwa Kimatira kabla ya kuchukua hatua za kudhibiti. Hufyonza vikonyo vya maua na kusababisha kubadilika rangi kuwa nyeusi.

MADHARA YAKE.

. Husababisha kukauka kwa maua na kupukutika kwa matunda.

. Mashambulizi haya pia huingiza ugonjwa wa ukungu ambao huozesha kahawa na kuwa mapepe, hivyo hupunguza ubora na wingi wa mavuno.

NAMNA YA KUMDHIBITI KIMATIRA.

. Pogolea matawi mara kwa mara kadri inavyoshauriwa.
. Punguza kivuli cha miti na nigomba.
. Tumia Fenitrothion 50% EC millilita (cc) 25 za dawa kwa lita 15 za maji, Selecron 720% EC millilita (cc) 25 za dawa kwa lita 15 za maji.
. Hakikisha shamba lako linakuwa safi kila wakati ili kuzuia kuzaliana kwa mdudu huyu.
. Dhibiti wadudu hawa mara tu wanapoonekana wastani wa kimatira wawili au watatu kwa mti shambani mwako.
. Ni muhimu mashamba ya majirani yakadhibitiwa kwa wakati mmoja na shamba lako.

FAIDA ZA KUMDHIBITI KIMATIRA.

Mkulima akimdhibiti kimatira atapata faida zifuatazo;

. Atakuwa amepunguza kuzaliana kwa wadudu.
. Atakuwa ameongeza mavuno na ubora wa kahawa.
. Atakuwa amejiongezea kipato chake na kuwa maisha mazuri zaidi.
. Atakuwa ameongeza pato la taifa kwa ujumla.

2. BUNGUA MWEUPE (MAPEMBE).

Bungua mweupe au " Mapembe" ana mabawa yenye magamba meusi na kijivu. Pia ana kipapasi kirefu (antena). Wiki 1 hadi 2 baada ya mvua za vuli kuanza, mdudu huyu hutoka ndani ya shina la kahawa na kujilisha kwenye magamba machanga au matunda ya kahawa. Uharibifu wake wakati huu ni mdogo. Mdudu huyu hutaga mayai chini ya magamba kwenye shina la kahawa sentimita 30 kutoka usawa wa ardhi. Mayai huanguliwa baada ya wiki tatu na kuwa kiwavi ambaye huanza kujilisha kwa kuparua magamba ya kahawa kabla ya kutoboa na kuingia ndani ya mti ambapo hukaa kwa miaka miwili. Bila ya kumdhibiti mdudu huyu anaweza kusababisha hasara kwa kufyonza virutubisho na kufanya mti wa kahawa kuwa wa njano na baadaye kufa.

HATUA HATARI ZA MAPEMBE.

Hatua ya kiwavi cha mdudu huyu ndicho kinachosababisha madhara makubwa kwenye mti wa kahawa.

Dalili zake:
. Miti iliyoshambuliwa inakuwa na matundu kwenye mashina na hasa katika sehemu ya chini ambapo unga unga wa njano huonekana.
. Majani ya mti ulioshambuliwana kuathirika sana, hugeuka rangi ya njano na hatimae hunyauka na kufa.

Namna ya kumdhibiti:

. Njia muhimu ya kumdhibiti Mapembe ni kuutunza mti wa kahawa kuwa na afya nzuri kwa kupanda kwa nafasi iliyopendekezwa, kuweka mbolea ya kutosha, kuweka shamba katika hali ya usafi na kudhibiti wadudu na magonjwa.

. Baada ya kuvuna, kwangua magamba ya shina la kahawa (usawa wa goti toka ardhini) kwa kutumia gunzi la mahindi, ili kupunguza mazalia ya mdudu huyu, pia hufanya mayai na viwavi vyake kuonekana kwa urahisi na kushambuliwa na wadudu maadui wa mdudu huyu.

. Ua kiwavi wa bungua mweupe kwa kumchokonoa kwa waya ndani ya shimo.

. Vutia sisimizi watakao mla bungua kwa kuweka mafuta ya wanyama kwenye tundu.

. Kata miti iliyoshambuliwa sana (stumping), na kama lava amepekecha kuelekea chini, mtoe kwa waya.

. Paka chokaa, udongo au majivu ili kukausha mayai yasianguliwe kwenye shina na matawi.

. Nyunyiza mkojo wa ng'ombe uliovundikwa kwa siku 14 ili kuua au kufukuza wadudu hao.
. Kagua shamba na kamata na kuwaangamiza hasa mvua za vuli zinapoanza.

Mambo muhimu ya kuzingatia:

Ni muhimu mashamba ya jirani yakadhibitiwa kwa wakati mmoja ili kuzuia mapembe kuhamia mashamba hayo.

3. RUHUKA.

Ruhuka ni mdudu hatari ambaye huishi kwenye mibuni na mimea jamii ya mikunde, ambayo huwa ni mbadala wakati matunda ya kahawa hayapo. Mdudu huyu hushambulia zaidi mibuni aina ya Robusta na Arabica kwenye ukanda wa chini. Madhara ya mdudu huyu huendelea mpaka ghalani. Asipodhibitiwa anaweza kusababisha uharibifu wa zao shambani mpaka asilimia 90.

Dalili muhimu, uharibifu na madhara yake:

. Matunda mabichi au yaliyoiva huwa na tundu moja au zaidi kwenye kitovu cha tunda.

. Punje zilizoshambuliwa hubadilika rangi na kuwa kijani cha bluu. Katika hali hii viwavi huwepo ndani ya punje.

. Matundu yaliyotobolewa huweza kuwa njia ya kupenyeza ukungu na bacteria na kupunguza ubora wa zao.

. Ruhuka huendelea kushambulia punje ghalani na hivyo kushusha ubora wa kahawa.

Namna ya kumdhibiti Ruhuka:

. Epuka kuotesha miti ambayo inaficha hawa wadudu wakati usio msimu kama Lantana camara.

. Punguza kivuli cha shambani.

. Pogoa matawi inavyoshaushauriwa.

. Chuma kahawa mara kwa mara (kila baada ya siku 14) ili kahawa isikauke juu ya mti na hivyo kuzuia masalia ya matunda yenye Ruhuka.

. Okota matinda yote yaliyoanguka shambani wakati wote, na ondoa matunda yote yaliyobaki kwenye kahawa baada ya msimu. Chimba shimo na ufukie matunda hayo. Kwa kufanya hivyo unakatisha mzunguko wa maisha ya ndudu huyu.

. Weka matandazo ili kuendeleza wadudu marafiki wanaokula Ruhuka, hii pia husaidia kuozesha matunda yaliyodondoka chini.

. Chunguza kuwepo kwa Ruhuka katika miezi ya Februri na Machi. Akiwepo nyunyizia dawa za asili kama mwarobaini na utupa. Uchunguzi ukionyesha kuendelea kuwepo kwa Ruhuka, nyunyizia sumu za viwandani kama vile Thiodan 35EC au Dursban 48EC (15mls kwenye lita 20 za maji). Hii ifanyike kabla ya Ruhuka kuingia ndani ya punje.

. Tumia njia za kiasili kumdhibiti Ruhuka kwa mfano mtego wa chupa kwa kutumia kileo kama vile gongo, mbege, rubisi na konyagi.

. Hakikisha kwamba dawa inapigwa miezi 4 kabla ya kuvuna kahawa. Ni vyema mashamba ya majirani pia yadhibitiwe kwa wakati mmoja na shamba lako.

Faida za kumdhibiti Ruhuka:

. Kuongeza wingi wa kahawa.
. Kupunguza hasara na kuongeza kipato.
. Kupunguza uwezekano wa kupata sumu ya ukungu (OTA).

4. KIDOMOZI.

Kidomozi ni nondo mdogo mweupe ambaye mchana hujificha chini ya majani ya kahawa na kuruka usiku. Kidomozi hushambulia zaidi majani ha kahawa aina ya Arabika. Mashambulizi yanayofanywa na wadudu hawa hupunguza mazao kwa asilimia 8-10. Nondo wa kidomozi hutaga mayai juu ya majani ya kahawa na huangua viwavi wadogo ambao huharibu mjani kwa kuacha makovu ya kahawia.

Dalili zake:
. Majani yaliyoshambuliwa yanakuwa na mabaka ya rangi ya kahawia na juu ya jani linaonekana lina mabaka ya ukavu.

. Endapo ukifumua kovu kwa kutumia waya mwembamba utaona viwavi wembamba na weupe.

Madhara yake:

. Mashambulizi ya viwavi hawa hupunguza eneo la majani linalotengeneza chakula cha mmea na kusababisha majani kupukutika.

. Kupukutisha majani husababisha mti wa kahawa kushindwa kutengeneza chakula cha kutosha kujilisha na hasa kulisha matunda.

Namna ya kumdhibiti kidomozi:

. Zingatia usafi wa shamba (kukata matawi, kukatua shamba na kuweka matandazo).

. Punguza kivuli shambani ili mwanga wa jua upenye kwa asilimia 60.

. Tumia dawa ya asili kama mkojo wa ng'ombe kwa uwiano wa 1:4 (mkojo:maji) kwa kunyunyizia kwenye shamba la kahawa.

. Tumia Selecron 720EC cc 25 za dawa kwenye lita 15 za maji, Dursban 48%EC tumia cc 30 za dawa kwa lita 15 za maji. Decis (Deltamethrin) 2.5%EC tumia cc 6.5 kwa lita 15 za maji, Furadan 5G (Carbofuran) tumia gram 30 kwa mti kila mwanzoni mwa mvua (Dawa hii ya carbofuran iwekwe chini kwenye mizizi).

. Dawa hizi zitumike wakati nondo 30 au zaidi wanapoonekana kwenye mti.
. Tumia dawa hizi baada ya wiki moja nondo wa mdudu huyu wanapokuwa wengi. Rudia tena kupiga dawa baada ya wiki 2 hadi 3.

. Badilisha dawa za kudhibiti mara kwa mara kwani utumiaji wa aina moja ya dawa husababisha wadudu hawa kuwa sugu.

Faida za kumdhibiti kidomozi:

Mkulima akidhibiti kidomozi atapata faida zifuatazo:
. Atakuwa amepunguza kuzaliana kwa wadudu hawa
. Atakuwa ameongeza wingi wa mavuno na ubora wa kahawa.
. Atakuwa amejongezea kipato chake na kuwa na maisha mazuri zaidi.
. Atakuwa ameongeza pati la taifa kwa ujumla.

6. UWIWI.

Ni mdudu msumbufu wa maeneo ya nyanda za chini kwa hapa kwetu Tanzania. Hushambulia matunda na kuyachubua huku akifungamanisha matunda kadhaa kwa utando wa kahawia. Matunda hutobolewa na kukaushwa. Huweza pia kutoboa na kuharibu sehemu za juu zinazokua za matawi.

Kumdhibiti:
. Usafi wa shamba.
. Kukata matawi.
. Kuokota na kufukia matunda yaliyoharibiwa na yaliyofungamanishwa.
. Kuweka matandazo.
. Madawa yafaayo ni sawa na yale yaliyoainishwa kwa udhibiti wa kidomozi hapo juu.

7. BUNGUA NJANO.

Hushambulia majani hadi shina na kuathiri usafirishaji wa virutubisho, afya ya mti pamoja na mavuno. Dalili zake ni kunyauka sehemu za juu za matawi, matundu mengi madogo madogo kwenye tawi, matawi kuwa dhaifu na kuvunjika hasa kama yamezaa sana.

Kumdhibiti:
. Usafi wa shamba.
. Kuondoa matawi yaliyoathirika na kuyachoma au kuyafukia.
. Kuchokonoa matundu ya chini.
. Dawa asilia kama Utupa na Mwarobaini, na za viwandani kama Ultracide na Decis.

8. VITHIRIPI.

Hawa huweza kuwa tishio wakati wa ukame wa muda mrefu. Hushambulia sehemu zote laini za mmea (majani, vitawi vichanga na matunda) kwa kufyonza chembechembe hai. Majani yaliyoathirika yana rangi ya shaba juu na chini.

Kuwadhibiti:
. Usafi wa shamba.
. Kuweka matandazo, kivuli na kumwagilia maji ipasavyo.
. Piga dawa pale tu ukiona vithiripi watatu kwa jani. Waweza kutumia Selecron 50EC, millilita 50 kwa lita 15 za maji, utupa au mwarobaini.

Makala hii nimeiandaa kwa msaada wa kitaalam zaidi kutoka katika Taasisi ya uendelezaji na uboreshaji wa zao la kahawa Tanzania (TaCRI), kituo cha Mbimba- Mbozi, Mbeya.

Ahsanteni sana!

Imetayarishwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi- Agriculture Extension Field Officer at Mbozi District, Mbeya.

Sunday, March 2, 2014

UTUNZAJI WA VIFARANGA

Habarini ndugu zangu wakulima, wafugaji na watembeleaji na wapenzi wa blogu hii. Leo ningependa tujulishane na kufundishana juu ya ufugaji wa kuku na hasa tutajikita na utunzaji wa vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa yaani kuanzia siku ya kwanza kutoka kwenye yai mpaka siku ya tisini (90), miezi mitatu.

Hebu tuanze kwanza na hatua ya kwanza kabla vifaranga havijafika.

UTAYARISHAJI WA BANDA.

1. Banda liwe safi
2. Pulizia dawa ya kuondoa viroboto, utitiri na chawa kwa kutumia Ectomin dip.
3. Dawa ya kudhibiti wadudu wasababishao magonjwa tumia disinfectant aina ya Vivid/ YH4.
4. Tayarisha taa na moto (charcoal) kwa ajili ya kuweka chumba kiwe na joto la kutosha.

Siku ya 1.
i) Vifaranga wanapofika tu wapewe Glucose kwenye maji kwa masaa 8 mfululizo. Baada ya masaa 4 ya mwanzo ya glucose wapewe pamoja na chakula.

ii) Baada ya hapo wapatiwe Vitalyte kwa siku 2 mfululizo.

Siku ya 3.
Wapewe chanjo ya Newcastle Vaccine kwa saa 2 mfululizo. Baada ya hapo wapatiwe Vitalyte au Antisyress kwa diku 3 mfululizo.

Siku ya 7.
Wapewe chanjo ya Gumburo Vaccine kwa saa 2 mfululizo. Baada ya hapo wapatiwe maji ya Antistress kwa siku 2 mfululizo.

Siku ya 10.
Wapatiwe OTC Plus kwa siku kwa saa 24 kwa siku 3 mfululizo.

Siku ya 14,18,19.
Wapatiwe Esb3 na Vitalyte kwa masaa 24 kwa siku 3 mfululizo.

Siku ya 21.
Wapewe Newcastle Vaccine kwa saa 2 mfululizo. Baada ya hapo wapatiwe Antistress kwa siku 4 mfululizo.

Siku ya 28.
Wapewe Gumburo (booster) kwa masaa 2 mfululizo. Baada ya hapo wapatiwe Antistress kwa siku 2 mfululizo.

Siku ya 31.
Wapatiwe OTC Plus kwa siku 7 mfululizo.

Siku ya 43,44,45.
Wapatiwe Ecb3 na Vitalyte kwa masaa 24 mfululizo kwa siku 3.

Siku ya 50.
Wapewe chanjo ya Fowl Pox. Baada ya hapo endelea kuwapa Chickmycine au Chick Plus kwa wiki 2.

Siku ya 65.
Chanjo ya Gumburo na baada ya hapo endelea na Antistress.

Sku ya 69.
Wapatie dawa ya minyoo Levalap kwa siku 2 mfululizo.

Siku ya 72.
Wapatiwe Fluquin kwa siku 5 mfululizo.

Siku ya 79.
Wapatiwe Anticox na Vitalyte kwa siku 5 mfululizo.

Siku ya 90.
Wapewe tena chanjo ya Newcastle Vaccine kwa saa 2 mfululizo. Baada ya hapo endelea kuwapa Antistress kwa siku 3 mfululizo.


Baada ya siku hizo 90, endelea kuwapa chanjo ya Newcastle kila baada ya miezi 3 pamoja na kuwapa tiba ya magonjwa mbalimbali yanayowakabili mara kwa mara. Pia tafuta ushauri kwa wataalan mara tu uonapo tatizo kwa kuku wako.

Ahsanteni sana na karibuni muweze kuelimika. Toa maoni yako.