Thursday, February 27, 2014

SEMINA ELEKEZI YA MIKOPO YA PEMBEJEO CHINI YA AGRA

Ili kufanikiwa katika kilimo kunahitajika Pembejeo bora mashambani. Pembejeo hizo zinahitaji fedha, na wakulima wetu wengi ni wakulima wadogo wadogo (smallholders farmers) ambao kila mwaka wanadunduliza hapa na pale kujitafutia pembejeo na mara nyingi hazitoshelezi kumudu mashamba yao.

Kwa kuliona hilo, watafiti (Researchers) kutoka katika kituo cha utafiti Uyole (ARI-Uyole) chini ya Mtafiti William Mmari wameweza kuja na mradi ambao unadhaminiwa (funded) na Agriculture Green Revolution for Africa, AGRA, chini ya mwenyekiti wake Koffii Annan. Mradi huu unafanya mambo mengi kwa mkulima huyu mdogo mdogo na kati ya mambo hayo ni "Mikopo ya Pembejeo kwa Wakulima". Mkulima anakopeshwa pembejeo ya kutosha kuhudumi ekari moja ama ya Mahindi au Maharage, kisha atarejesha mkopo huo wakati wa mavuno na riba kidogo ya uendeshaji ambayo si kubwa ya kumuumiza mkulima.

Katika kuongeza ufanisi wa mradi huo wa mikopo ya pembejeo kwa wakulima, ARI-Uyole wamewaita kuwapa mafunzo wataalam wa kilimo (Extension Officers) wa kata na vijiji vinavyoguswa na mradi kutoka katika wilaya za Mbozi na Mbeya vijijini. Mafunzo hayo yalichukua siku mbili yakilenga hasa kuzijua mbinu njia ambazo mkulima huyu aliyekopeshwa pembejeo aweze kuzalisha vizuri na kurudisha mkopo wote na yeye kubakiwa na ziada.

Washiriki walijifunza kwamba, ili mkulima aweze kuhudumia shamba vizuri, ni lazima ajiwekee akiba ambayo itamsaidia katika manunuzi ya pembejeo wakati wa kulima. Mkulima ashauriwe kujiunga na vikundi vya wakulima vya kuweka na kukopa kama, AMCOS, ambavyo kwa sasa vimesamba sana huko vijijini na wamiliki ni wakulima wenyewe.

Katika hali ya kawaida uzoefu unaonyesha kwamba, watu wengi wana fikra ya msaada (kusaidiwa) katika akili zao. Hili linadhoofisha sana Mikopo hasa hii ya Pembejeo. Ili kudhibiti hilo Mikopo ya Pembejeo ya AGRA inapitia kwa wanachama hai kwenye AMCOS na wataunda vikundi vidogo ndani mwao ili waweze kujisimamia.

Matarajio ya Mradi ni kumjengea uwezo mkulima ili aweze kujiendeleza mwenyewe na apanue kilimo chake.

Tuesday, February 18, 2014

MBOGA ZA MAUA: 2 BROKOLI.

Zao hili nalo pia ni geni katika nchi hii, lakini kwa kuwa linaendelea kulimwa na hupendwa na wakazi wengi, ni vizuri kuelewa jinsi ya kulistawisha.

Igawa zao lilistawishwa tangu zama za Warumi, ni katika karne hii tu ambapo limeenezwa na kutumiwa katika sehemu nyingi duniani. Kwa sasa mboga hii hustawishwa sana katika nchi nyingi za tropiki, hasa Afrika na Visiwa vya Caribbean.

Brokoli ina kiasi kikubwa cha Vitamini A. Sehemu inayotumiwa ni kichwa au ua la mmea ambalo kidogo hufanana na koliflawa. Tofauti kubwa ni kwamba tunda lake ni mkusanyiko wa vichwa au ni shada la maua madogo madogo yaliyokusanyika pamoja bila ya kubanana sana. Rangi ya matunda ni kijivu-kijani, au kibluu-kijani, au kijani iliyofifia. Brokoli huchukua muda mrefu zaidi kukua na kukomaa kuliko kabeji.

AINA: Kama yalivyo mazao mengine, pia kuna aina kadhaa za zao hili ambazo hupendelewa zaidi na wakulima au walaji, kwa mfano Calabrese, De Cicco, Texas 107, Carvet Hybrid, Barca Hybrid, Green Sprouting na Mountain.

Wakati wa kuvuna, ua lote hukatwa pamoja na sehemu ya juu ya shina ambayo ni laini. Vile vile unaweza kuongeza kidogo cha majani yazungukayo ua. Mapishi na matumizi yake ni sawa na ya kabeji au koliflawa; yaani huchemshwa na kutengenezewa mchuzi, au kufanywa supu na rojorojo.

USTAWISHAJI: Brokoli huweza kustawi katika sehemu ambazo koliflawa hustawi, lakini ina uwezo mkubwa zaidi wa kuvumilia joto na uhaba wa mvua. Ili kupata matunda makubwa, ni muhimu kuhakikisha kwamba matunda hayo yanavunwa nyakati za baridi. Hii ni kwa kuwa hali ya joto husababisha matunda kukua kwa haraka mno kiasi kwamba ni vigumu kufuata utaratibu wa kuyavuna kidogo kidogo na kwa wakati unaostahili. Hakikisha udongo hautepeti na kutuamisha maji. Unaweza kuongeza mavuno kwa kuweka mbolea ya Nitrogen (Sulphate of Ammonia).

MAGONJWA: Magonjwa na wadudu washambuliao zao hili ni sawa na wa kabeji na koliflawa.

KUVUNA: Kwenye sehemu za joto tunda la kwanza huvunwa siku 60-70 tangu kupandikizwa. Na kwa nyanda za juu, siku 100-120.

Ahsanteni!

Thursday, February 13, 2014

MBOGA ZA MAUA 1. KOLIFLAWA

Zao hili hustawishwa kwa ajili ya kichwa au ua lake ambalo kwa kawaida ni jeupe na gumu. Ustawi wake karibu ni sawa na kabeji. Ingawa koliflawa (cauliflower) ni mboga nzuri na inayojulikana na kutumiwa kwa wingi, hutumiwa sana pia na nchi nyingi duniani.

Mmea wa koliflawa huweza kukaa bustanini kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini kwa kawaia hulimwa na kuvunwa kila mwaka. Kitumiwacho katika mmea huu ni kichwa au ua lake ambalo kidogo ni mviringo, jeupe na gumu. Wakati wa kukua ua au tunda hufunikwa na majani ya mmea. Ukubwa wa tunda hutegemea hali ya udongo na hewa, pamoja na aina ya mbegu. Tunda lake huliwa baada ya kuchemshwa, pia huweza kuachanganywa mboga nyingine au kwenye supu na achali.

Zipo aina nyingi za mboga hii ambazo hupendwa zaidi. Aina hizo hutofautiana kwa ukubwa wa mimea, ukubwa wa matunda, ugumu wake, umbo lake, muda wake wa kukomaa, wingi wa majani na kadhalika.

Miongoni mwa aina za koliflawa ambazo hujulikana zaidi ni: Early Patma, Early Maket, snowball, white Mountain, Kibo Giant, Southern cross.

Zao hili hupendelea hali ya baridi kiasi na unyevu mwingi. Hushindwa kuvumilia hali ya baridi sana au joto jingi. Katika sehemu zilizo na joto kali, matunda ya koliflawa huwa madogo mno, kwa hivyo, ni sehemu chache nchini mwetu ambako zao hili linaweza kustawi vizuri. Hata hivyo utafiti na majaribio yanaendelea kufanywa ili kuweza kupata aina zenye uwezo wa kustawi katika hali ya tropiki.

Koliflawa huchukua kiasi kikubwa sana cha chakula kutoka ardhini, hivyo licha ya kurudishia mbolea, pia baada ya kuvuna inashauriwa kupanda mimea isiyotumia chakula kingi, kama kunde, maharage.

Koliflawa huwa tayari kuvunwa baada ya majuma 10 hadi 18 tangu kupandikizwa bustanini. Muda wa kukomaa hutegemea aina ya mimea na hali ya hewa kwani huchelewa zaidi katika hali ya baridi sana. Matunda yavunwe kabla hayajalegea na kuanza kupoteza rangi yake.

Magonjwa yashambuliayo:
Damping Off, Black Rot, Stem Rot.

Ahsanteni sana.

Prepared by:

Marcodenis E. Misungwi 

Agriculture Field  Extension Officer.